Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimnataifa wa Akili Mnemba mjini Shanghai, China, Ijumaa Julai 16 kwa saa za huko, Katibu Mkuu amesema AI ina uwezo wa kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), lakini hilo litawezekana tu ikiwa kila nchi itapata fursa sawa ya kushiriki katika maendeleo na matumizi ya teknolojia hiyo.

“Teknolojia lazima iwahudumie watu, si watu kuitumikia teknolojia,” amesema.

Kupunguza pengo la AI

Guterres ameonya kuwa licha ya uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi katika AI, nchi nyingi zinazoendelea bado zinakabiliwa na changamoto za miundombinu ya mawasiliano, uwezo wa kompyuta, upatikanaji wa data na utaalamu wa kiufundi, hali ambayo inaweza kuongeza zaidi pengo kati ya nchi tajiri na maskini.

Amebainisha kuwa takribani theluthi moja ya watu duniani bado hawajaunganishwa na mtandao na kusisitiza kuwa usimamizi wa AI haupaswi kuachiwa mataifa machache au kampuni chache, bali unapaswa kuwashirikisha wote kupitia Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali na Majadiliano ya Kimataifa kuhusu Usimamizi wa AI yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Vipaumbele vitatu

Katibu Mkuu ametaja maeneo matatu ya kipaumbele ili kuhakikisha kila nchi inanufaika na mapinduzi ya AI:

  • Kujenga uwezo: Kusaidia nchi zinazoendelea kupata mifumo nafuu ya kompyuta, miundo ya AI iliyo wazi, mafunzo na teknolojia inayokidhi mahitaji na lugha zao.
  • Usalama: Kuweka viwango vya kimataifa vya upimaji, tathmini ya hatari na usimamizi wa AI, huku haki za binadamu zikilindwa na maamuzi ya uhai na kifo yakibaki mikononi mwa binadamu.
  • Uendelevu: Kupunguza athari za AI kwa mazingira kwa kuongeza matumizi ya nishati jadidifu na kuzitaka kampuni kubwa za AI kuweka wazi athari za kimazingira za mifumo yao.
  •  

Mipango mipya ya Umoja wa Mataifa

Guterres amesema zaidi ya nchi 20, ikiwemo China, tayari zimependekeza vituo vyao kujiunga na Mtandao wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa Kubadilishana Uzoefu na Ushirikiano wa Kujenga Uwezo wa AI. Pia ametangaza kuwa hivi karibuni atawasilisha mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Kimataifa wa AI, akitoa wito kwa mataifa kuunga mkono juhudi hizo.

Akihitimisha hotuba yake, Katibu Mkuu amesema swali muhimu si kama AI itabadilisha dunia, bali ni kama mabadiliko hayo yatapunguza ukosefu wa usawa au yatauzidisha.

“Hili ni jaribio la teknolojia na pia jaribio la mshikamano,” amesema, akizihimiza nchi kushirikiana ili kuhakikisha AI inakuwa “nguvu ya kuleta utu, fursa na maendeleo endelevu kwa wote.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *