Jeshi la Sudan limetangaza kuuawa kwa idadi kubwa ya wapiganaji wa kigeni, wakiwemo mamluki wa Kiukraine, waliokuwa wakiunga mkono kikosi cha waasi cha Rapid Support Forces (RSF) katika vita vya muda mrefu vya ndani nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Sudan (SAF), mauaji hayo yalitokea wakati wa mapambano makali na RSF katika jiji lililozingirwa la El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini. Operesheni hiyo maalum, iliyoendeshwa na Kikosi cha 6 cha Miguu cha SAF kwa kushirikiana na vikosi washirika, ilisababisha hasara kubwa kwa RSF, ikiwa ni pamoja na vifo na uharibifu wa vifaa vya kijeshi.

SAF ilieleza kuwa mamluki kutoka Colombia na Ukraine, wakiwemo wahandisi wa teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drones) na mifumo ya kielektroniki, walijaribu kuingia kwa siri katika vitongoji vya jiji hilo.

Mapigano makali nchini Sudan yalianza Aprili 2023, kati ya mkuu wa SAF, Abdel Fattah al-Burhan, ambaye pia ni kiongozi wa Sudan na kamanda wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo (maarufu kama Hemedti). Wawili hao walikuwa wakishirikiana madaraka katika serikali ya mpito iliyoundwa baada ya maandamano ya mwaka 2019. Kinara wa RSF anataka kunyakua madaraka kikamilifu huku mpito wa kuelekea utawala wa kiraia ukiwa umekwama.

Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa Sudan inakabiliwa na janga baya zaidi la kibinadamu duniani, ambapo maelfu wameuawa na nusu ya raia wanakabiliwa na njaa kali kutokana na vita vya mzingiro, mashambulizi dhidi ya maeneo ya kiraia, na njia za misaada kufungwa. Kufikia Septemba, takriban watu milioni 12 walikuwa wamelazimika kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa UN.

Serikali ya mpito ya Sudan imekuwa ikilalamikia kwa muda mrefu kuingilia mataifa ya kigeni katika mgogoro huo. Mnamo Agosti, jeshi la anga la Sudan lilisema kuwa liliharibu ndege ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) iliyokuwa imebeba wapiganaji wa Colombia katika uwanja wa ndege unaoshikiliwa na RSF huko Darfur, na kuua watu wasiopungua 40 waliokuwa ndani.

Mwezi Juni, afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan aliambia RT kuwa Ukraine pia ilikuwa ikiipatia RSF silaha. Alisema kuwa Kiev ilikuwa ikifanya “kazi chafu” ya mataifa ya Magharibi kwa kusaidia makundi ya waasi yanayohusishwa na mashambulizi ya kigaidi nchini Libya, Somalia na Niger.

Serikali za kijeshi za Burkina Faso, Mali, na Niger pia zimeishtumu Ukraine kwa kusaidia “ugaidi” katika ukanda wa Sahel, na kwa pamoja zimewasilisha malalamiko kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ukraine imekanusha tuhuma hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *