Dar es Salaam. Mchakato wa maridhiano unaoendelea Visiwani Zanzibar kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo umeibua upya mjadala wa Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ndani ya Muungano, dai ambalo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema lina ugumu katika utekelezaji.

Viongozi wa ACT wameibuka wakisisitiza kuwa ajenda ya maridhiano haiishii kwenye ushirikiano wa kisiasa pekee, bali inalenga pia mustakabali wa Zanzibar, likiwemo la kuwa na mamlaka kamili.

Katika mkutano uliofanyika Alhamisi, Julai 16, 2026, Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, akiwa pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman (OMO), alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kusimamia ajenda hiyo kama sehemu ya maridhiano yake na CCM kwa masilahi ya Wazanzibari.

“ACT-Wazalendo tunafahamu na tutasimamia hitaji la Wazanzibari kuwa na Zanzibar yenye mamlaka kamili,” alisema Mchinjita baada ya kuwahoji wananchi waliokuwa wamekusanyika katika mkutano huo.

“Wazanzibari mnataka nini?” alihoji Mchinjita na kujibiwa na wananchi katika mkutano huo, “mamlaka kamili.”

Kwa upande wake, OMO alisisitiza kuwa ACT haiingii katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutafuta vyeo, bali kutafuta suluhisho kwa masuala yanayoihusu Zanzibar.

OMO alieleza kuwa ACT inataka kupitia na kurekebisha baadhi ya vipengele vya Katiba ya Zanzibar ambavyo chama hicho kinaamini vinakuwa kikwazo katika kasi ya maendeleo na utekelezaji wa mamlaka ya Zanzibar.

Suala la mamlaka kamili ya Zanzibar limekuwa ajenda ya muda mrefu ya Wazanzibari na limekuwa likisukumwa zaidi na vyama vya upinzani vya CUF na sasa ACT-Wazalendo.

Lilijitokeza zaidi wakati wa mchakato wa Katiba Mpya ya Muungano wa mwaka 2012 hadi 2014.

Hata hivyo, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 katika Ibara ya Kwanza inasema: Zanzibar ni Nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Ibara ya Pili inasema:  Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Si hoja ngeni

Hoja ya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ina historia ndefu katika siasa za visiwa hivyo. Tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Zanzibar iliendelea kuwa na Serikali yake ya Mapinduzi, Baraza la Wawakilishi na Katiba yake, huku masuala ya Muungano yakisimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, mbali na kuitambua kama nchi, Katiba ya Zanzibar pia imeweka msingi wa uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mamlaka katika mambo yasiyo ya Muungano.

Ibara ya 3(2) inasema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa na uwezo wa kuweka kitu chochote kitakachokuwa kielelezo cha Serikali kama itavyokubaliwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Hata hivyo, mjadala wa muda mrefu ni kuhusu mipaka ya mamlaka hayo, hasa kwa maeneo ambayo baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Zanzibar wameona yanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi ya kujiamulia mambo.

Miongoni mwa waliowahi kubeba kwa muda mrefu hoja hiyo ni Maalim Seif Sharif Hamad, mwanasiasa aliyekuwa mmoja wa waasisi wa upinzani Zanzibar na baadaye kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia maridhiano ya kisiasa.

Katika uongozi wake ndani ya CUF na baadaye ACT-Wazalendo, Maalim Seif aliendelea kuzungumzia Zanzibar kuwa na nafasi pana zaidi katika kuendesha mambo yake, hoja iliyojikita katika madai ya Zanzibar kuwa na uwezo wa kusimamia rasilimali zake, uchumi wake na masuala yake ya ndani bila vikwazo vya kikatiba kimuungano.

Maalim Seif alishiriki mazungumzo ya kisiasa, kujenga maridhiano na kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hatua ambayo kwa sasa inasimamiwa na ACT-Wazalendo chini ya OMO kama sehemu ya maridhiano, huku wakiendelea kusukuma ajenda ya mamlaka kamili.

Sasa, kupitia ACT-Wazalendo, ajenda hiyo imeanza kupewa msukumo mpya ikihusishwa na dhana ya maridhiano.

Ugumu wa utekelezaji

Licha ya msukumo huo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema utekelezaji wa suala hilo una ugumu kwa kuwa linagusa moyo wa Muungano na hivyo kuhitajika mchakato mpana wa kulifikia.

Akifafanua hilo, mchambuzi wa masuala ya siasa Visiwani Zanzibar, Profesa Mohamed Makame amesema suala hilo limekuwa gumu kwa kuwa si la wanasiasa pekee, bali ni suala la kisheria na la wananchi wote kwa kuwa linagusa mifumo ya Katiba.

“Nikweli ajenda hii imekuwa ikijitokeza kwa muda mrefu, hata Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ilikuja na jambo hili kutokana na maoni ya wananchi. Muungano huu umeundwa kikatiba kupitia vyombo vikuu vya utungaji sheria, mabadiliko yoyote lazima yatokane na mchakato wa maridhiano kama huo,” amesema.

Ingawa wapo baadhi ya makada wanaozungumzia suala hilo, Profesa Makame amesema halipaswi kuwa ajenda ya upinzani tu au upande mmoja wa Muungano pekee bila pande zote kulizungumza kwa kina.

“Busara iliyotumika mwaka 1964 ni nchi mbili kujivua mamlaka yake na kuunda nchi moja, Zanzibar ikaachwa ibaki na sehemu ya mamlaka ikiwa na Rais, Baraza la Wawakilishi na Mahakama hadi Mahakama Kuu. Ingawa baadhi ya wananchi wamekuwa wakidai Zanzibar kuwa na mamlaka kamili, ninachokiona haiwezekani nchi moja kuwa na mamlaka kamili ndani ya Muungano wa nchi mbili,” amefafanua.

Amesema kuwa na Zanzibar yenye mamlaka kamili kutalazimisha kuundwa kwa nchi nyingine huru ya Tanganyika, akisema hatua hiyo haiwezekani. Badala yake, inaweza kuangaliwa kuongeza au kupunguza mambo ya Muungano badala ya nchi kujiengua na kuwa na mamlaka kamili.

“Huwezi kuwa na Muungano wa nchi mbili, moja iwe na mamlaka kamili na nyingine ijivue mamlaka yake. Suala hili linahitaji busara na utulivu mkubwa na ushiriki wa kila mmoja kwa namna Taifa la Tanzania litaendelea kuwa pamoja kwa kuangalia nini kinazaa hoja hizi bila kuathiri Muungano,” amesema.

Uchambuzi wa Profesa Makame unaendana na mawazo ya mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa na diplomasia, Deus Kibamba aliyesema kwa sasa ni vigumu kusukuma ajenda nyeti ya kitaifa kama hiyo, ikafanikiwa kutokana na hali ya mgawanyiko iliyopo katika jamii na kupungua kwa imani ya wananchi kwa viongozi wao.

Amesema uzoefu wa Zanzibar unaonyesha kuwa mafanikio ya maridhiano ya kisiasa hayakuja kwa urahisi, bali yalitokana na mchakato mrefu wa mazungumzo uliowashirikisha wadau mbalimbali.

Ametaja nafasi ya aliyekuwa kiongozi wa upinzani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, katika kuwezesha maridhiano yaliyozaa makubaliano ya kisiasa.

Kibamba amesema mazungumzo hayo yaliishia kuzaa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 na kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, mfumo ulioweka sharti kwamba chama kitakachoshika nafasi ya pili na kupata angalau asilimia 10 ya kura zote za urais kishiriki kuunda Serikali pamoja na chama kilichoshinda uchaguzi.

Amesema historia hiyo ni kielelezo kwamba kujenga maridhiano ya kweli kunahitaji muda, uvumilivu na ushirikishwaji mpana wa wadau wote wa kisiasa.

Kwa mujibu wa Kibamba, mazingira ya sasa yanayoonyesha jamii kugawanyika yanafanya iwe vigumu kwa viongozi kusukuma ajenda nyeti na zikapata uungwaji mkono wa wananchi.

“Kiwango cha wananchi kuwaamini viongozi wao kikishuka, mambo mengi hayawezi kufanikiwa. Mwanasiasa hata akitangaza jambo inakuwa ngumu kuungwa mkono,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, amesema suluhisho ni viongozi wa vyama vyote vya siasa kukaa pamoja na kufanya mazungumzo ya kina badala ya kuacha jukumu hilo kwa kundi dogo la watu.

“Jambo hilo halitafanikiwa ikiwa halitakuwashirikishi. Lazima viongozi wa vyama vyote, si kikundi cha watu wachache, wakae wazungumze, wamalize tofauti zao, kisha waunde Serikali ya pamoja itakayoaminiwa na wananchi wote. Bila hivyo hakuna jambo litakalowezekana,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *