
Mkuu wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) ametembelea kaskazini magharibi mwa Nigeria, wakati migogoro, umaskini na ukosefu wa usalama wa chakula vikiwalazimisha mamilioni ya watoto katika eneo hilo kuhitaji msaada ya dharura.
Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, jana Ijumaa alitembelea jimbo la Sokoto, ambapo shirika hilo linakusudia kuelekeza mazingatio yake kwenye changamoto zinazozidi kuwa mbaya zinazowakabili watoto.
Alikutana na maafisa wa serikali na kutembelea programu zinazoungwa mkono na UNICEF zinazolenga kuboresha afya ya akina mama na watoto na kuwalinda vijana walio katika mazingira magumu.
“Tunapaswa kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa katika migogoro hii,” amesema Catherine Russell baada ya kukutana na maafisa wa serikali na kutembelea programu zinazofadhiliwa na UNICEF zinazolenga kuboresha afya ya akina mama na watoto na kuwalinda vijana walio katika mazingira magumu.
Maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria tayari yanakabiliwa na mgogoro wa usalama ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu.
Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umezidisha ukosefu wa usalama wa chakula kwa mamilioni ya watu wanaoishi katika umaskini, na kuwafanya watoto katika kaya maskini kuwa katika hatari kubwa zaidi.
UNICEF inasema, watoto kati ya milioni 18.3 na 23.4 katika kaya maskini duniani kote wametumbukia katika umaskini mkubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na watoto milioni 6.5 hadi milioni 8.8 barani Afrika.
Nigeria ina mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya watoto maskini duniani, na mashirika ya kibinadamu yanaonya kwamba wale walio kaskazini mwa nchi hiyo iliyokumbwa na migogoro wanasalia kuwa miongoni mwa walio hatarini zaidi.