
KIKOSI cha Singida Black Stars, kitakuwa na sura nyingi mpya za wachezaji waliyosajiliwa, tayari wengine wameishaingia kambini na kufanya mazoezi ya kujiandaa na michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026, inayofanyika nchini Rwanda.
Chanzo cha ndani kutoka Singida BS kilitaja baadhi ya wachezaji wapya ambao wapo kambini kuwa ni Omary Omary aliyekuwa anacheza Mashujaa kwa mkopo kutoka Simba, kiungo Abdallah Hamisi kutoka Pamba na aliwahi kupita kwa Wanamsimbazi.
Wengine ni beki wa pembeni Nickson Mosha kutoka KMC, kiungo wa kati Emmanuel Mwanengo kutoka Yanga na Henry David kutoka Fountain Gate FC.
“Wengine ambao wapo kambini ni Yona Amosi kutoka Pamba, Shekhan Ibrahim Khamis kutoka Yanga, wengine tutakutana nao Rwanda kama Jonathan Sowah,” kilisema chanzo
“Kuhusu winga Ladaki Chasambi kutoka Simba inawezeka akajiunga na kambi hapa nchini ama tukakutana naye Rwanda, maana kuna vitu vichache ambavyo vinakamilishwa kuhusu yeye.”
Chanzo hicho kilisema licha ya kusajili wachezaji wapya wapo wengine ambao walimaliza mkataba yao.
”Kuna wachezaji wengine tutawatangaza kuwaacha na kuwatoa kwa mkopo.”