Dar es Salaam. Mgogoro wa kuuzwa nyumba ya makazi ya familia ya mfanyabiashara, Johan Harald Abrahamsson na hatimaye kuondolewa katika makazi hayo umechukua sura mpya baada ya mfanyabiashara huyo kuiburuta tena mahakamani Benki ya Exim (Tanzania) Limited na wenzake, kwa tuhuma za udanganyifu.

Nyumba hiyo ya kifahari iliyoko kitalu namba 16, Jangwani Beach, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, ilipigwa mnada mwaka 2017 kwa amri ya mahakama kulipia deni la Benki ya Exim lililotokana na mkopo wa Sh10 milioni ambao Abrahamsson aliidhamini kampuni ya Dascar Limited.

Amri hiyo ya mahakama ilitokana na maombi ya Exim ya utekelezaji wa hukumu ya kesi yake ya madai namba 51/2008 iliyoifungua dhidi Dascar Limited (mkopaji) na Abrahamsson (mdhamini wa mkopo huo); baada ya kushinda rufaa yake iliyoikata Mahakama ya Rufani.

Makazi hayo yanajumuisha nyumba moja ya ghorofa moja, yenye vyumba vya kulala vitano, vitatu vyenye vyoo na mabafu ndani (master bedrooms), viwili vya kawaida, sebule mbili, jiko na choo na bafu la jumuiya.

Pia kuna nyumba ndogo yenye vyumba vitano, viwili kati yake vyenye vyoo na mabafu ndani ‘masterbedroom’, vitatu vya kawaida na vyoo na mabafu mawili ya jumuiya, eneo la kuegesha magari na gereji yenye uwezo wa kuingia magari manne, pamoja na bwawa kuogelea.

Nyumba hizo zimejengwa kwenye eneo (kiwanja) lenye ukubwa wa mita za mraba 4303.

Kwa mujibu wa Abrahamsson kulingana na ripoti ya uthamini uliofanywa na Wizara ya Ardhi mwaka 2017, thamani yake katika bei ya soko ni Sh2.5 bilioni.

Hata hivyo, iliuzwa kwa Sh300 milioni tu, kufidia deni la Sh113 milioni zilizodaiwa kutokana na malimbikizo ya mkopo huo wa Sh10 milioni.

Miaka takribani tisa baada ya mapambano ya awali ya mahakamani bila mafanikio, Abrahamsson ameiburuta tena mahakamani Exim na wenzake akipinga amri za mahakama hiyo kukamata na kuiuza nyumba yake, akidai kuwepo udanganyifu na ukiukwaji sheria katika mchakato wa mnada huo.

Wajibu maombi wengine katika shauri hilo ni kampuni aliyoidhamini Abrahamsson kupata mkopo huo, Dascar Limited; dalali aliyeteuliwa kutekeleza amri za mahakama, Mas & Associates Company Limited and Court Broker na mnunuzi, Yusuph Shabani Matimbwa.

Katika shauri hilo la maombi mchanganyiko ya kibiashara namna 8901/2026, Abrahamsson anaiomba mahakama hiyo iridhie kuamua maswali yanayotokana na utekelezaji wa amri yake kuhusu utekelezaji wa hukumu hiyo.

Anadai amri hiyo ilitolewa bila kuzingatia nyumba hiyo ni ya wanandoa na makazi yake na familia yake ambao ni mkewe na watoto wao wawili wanayoitegemea.

Pia anadai amri hiyo ilipatikana kwa udanganyifu kwa Exim na bila kuzingatia uthamini wa nyumba hiyo ambayo thamani yake ilikuwa juu sana kuliko kiasi cha deni kilichokuwa kinadaiwa katika hukumu hiyo.

Abrahamsson anadai kuwa dalali huyo aliacha kutekeleza wajibu wake kama afisa wa utekelezaji amri ya mahakama, kwa kushindwa kuhakikisha kuwa thamani ya mali iliyotakiwa kuuzwa, kwa kadiri ilivyowezekana, inaendana na kiasi cha deni.

Anafafanua wakati deni lilikuwa Sh113,489,432 (zaidi ya Sh113.48 milioni), thamani ya mali hiyo ilikuwa Sh2.5 bilioni, kiasi  ambacho hakikukaribia kwa kadiri ilivyowezekana kuendana na kiasi kilichokuwa kinadaiwa katika hukumu iliyotekelezwa.

Vilevile anadai kuwa nyumba hiyo iliuzwa kinyume cha sheria na kwa udanganyifu kwa Matimbwa kwa thamani ya chini sana ya soko ya Sh300 milioni.

Anadai mauzo hayo haramu yanayolalamikiwa yamemsababisha yeye na familia yake madhara   ikiwamo ugumu wa maisha kwa kuwakosesha makazi na kumsababishia matatizo ya kiafya kutokana na msongo wa mawazo.

Hata hivyo, Exim imekanusha madai na tuhuma hizo za udanganyifu na ukiukwaji wa sheria, huku pia ikiibua pingamizi la awali ikidai kuwa shauri hilo limefunguliwa nje ya muda kwani lilipaswa lifunguliwe ndani ya siku 30 tangu tarehe ya mnada.

Pia inadai shauri hilo ni matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama kwani kuna shauri lingine Mahakama ya Rufani linalohusu masuala yanayoyalalamikiwa bado halijasikilizwa.

Matimbwa naye amekanusha madai na tuhuma hizo akidai kuwa nyumba hiyo haijawahi kuwa mali ya wanandoa wala makazi ya wanafamilia hao na hoja hiyo ilikwishakuamuliwa katika shauri lingine lililofunguliwa na mke wa Abrahamsson, Jacquiline, ambalo lilitupiliwa mbali.

Pia anakanusha kuwepo udanganyifu, vitendo visivyo halali au upotoshaji wowote katika mchakato wa utekelezaji wa hukumu ya kesi ya msingi, ama wakati wa mwenendo wa shauri mahakamani au wakati wa mnada wa hadhara.

Kwa mujibu wake mnada huo ulifanyika kwa mujibu wa sheria chini ya usimamizi wa Mahakama na kwamba umiliki wa nyumba hiyo ulishahamishwa kwa jina lake tangu Julai 5, 2018 na hati mpya ya umiliki ikatolewa kwa jina lake. 

Kisha mwaka 2023 aliiomba mahakama na akapata amri ya mahakama iliyoelekeza kuondolewa kwa watu waliokuwa wakiishi humo na kukabidhiwa yeye.

Abrahamsson alikata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi na amri hiyo, lakini Mahakama ya Rufani iliitupilia mbali Desemba, 2025.

Baada ya hukumu hiyo, alirudi (Matimbwa) Mahakama ya Biashara akaomba na mahakama hiyo itoe amri mpya ya kuondolewa kwa watu wote waliokuwa wanaishi katika nyumba hiyo.

Matimbwa anadai utekelezaji wa amri hiyo ulifanyika kwa utaratibu na kwa amani, na dalali aliyeteuliwa aliwasilisha taarifa yake mahakamani. 

Hivyo anapinga taarifa ya upekuzi (official search report) ankara za malipo ya kodi ya ardhi zilizoambatanishwa na Abrahamsson katika shauri hilo zinazoonesha kuwa umiliki wa nyumba hiyo bado haujabadilishwa.  

Badala yake anasisitiza kuwa umiliki wake ulishahamishiwa kwake, huku naye akiambatanisha na taarifa za upekuzi zinazoonyesha kwa sasa yeye ndiye mmiliki wa nyumba hiyo.

Majibizano hayo kupitia nyaraka za shauri hilo baina ya pande hizo mbili, yaani madai ya Abrahamsson, majibu ya Exim na pingamizi lake, majibu ya Matimbwa, na viambatanisho vilivyowasilishwa na pande zote kama vielelezo vinairejesha mahakama kwenye chimbuko la mgogoro huo.

Pia majibizano hayo na vielelezo hivyo ambavyo ni sehemu ya kumbukumbu za mahakama pia yanaibua utata wa baadhi ya mambo yanayolalamikiwa na Abrahamsson, ambayo ndio msingi wa simulizi hii, kama tutakavyoyachambua moja baada ya lingine.

Usikose kufuatilia simulizi hii hatua kwa hatua jinsi wema ulivyogeuka kuwa shubiri kwa Abrahamsson na familia yake kupoteza makazi yake na mvutano wa hoja za kisheria ulivyokuwa na unavyoendelea mpaka sasa.

Itaendelea kesho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *