Chanzo cha picha, Turkish Foreign Ministry handout/Anadolu via Getty Images
Kundi la wapiganaji wa Kipalestina Hamas limemchagua Khalil al-Hayya kuwa kiongozi wake mpya, anachukua nafasi ya Yahya Sinwar, ambaye aliuawa na jeshi la Israeli huko Gaza Oktoba 2024.
Hayya, ambaye ameliongoza kundi hilo la Gaza akiwa uhamishoni, anaonekana kuwa mtu wa msimamo mkali zaidi baada ya vita na Israeli vilivyoanza karibu miaka mitatu iliyopita. Alikuwa mshirika wa karibu wa Sinwar.
Akiwa mpatanishi mkuu wa Hamas, Hayya alipata umaarufu wa kimataifa kwa kuongoza ujumbe wa kundi hilo katika mazungumzo ya kusitisha mapigano yasiyo ya moja kwa moja na kukutana na wapatanishi nchini Misri na Qatar.
Hivi majuzi amepewa jukumu kubwa zaidi kasimamia mikakati ya kidiplomasia na kisiasa ya Hamas.
Septemba 2025, mzee huyo mwenye umri wa miaka 65 alinusurika shambulio la anga la Israeli lililolenga mkutano wa viongozi wa Hamas katika mji mkuu wa Qatar, Doha. Wanachama watano wa ngazi ya chini wa kundi hilo, akiwemo mmoja wa wanawe, waliuawa pamoja na afisa wa usalama wa Qatar.
Waziri mkuu wa Israeli alisema wakati huo kwamba Israel iliwalenga viongozi wa Hamas kwa sababu walihusika kupanga shambulio dhidi ya Israeli tarehe 7 Oktoba 2023, ambalo lilisababisha vita vya Gaza.
Wana wengine wawili wa Hayya waliuawa katika majaribio ya awali ya Israeli ya kumuua huko Gaza, huku wa nne akiuawa katika shambulio la anga la Israeli huko Gaza mwezi Mei.
Kuchaguliwa kwa Hayya kama mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas kulifuatia raundi mbili za upigaji kura.
Duru ya kwanza haikuwa na matokeo kamili, huku mkuu wa zamani wa ofisi ya kisiasa Khaled Meshaal akishinda kwa uchache kuliko Hayya, lakini alishindwa kupita kiwango kinachohitajika, kulingana na afisa mmoja wa Palestina mwenye ufahamu kuhusu uchaguzi huo.
Chini ya sheria za ndani za Hamas, mgombea lazima apate angalau kura 36 kutoka kwa wanachama wa tume ya uchaguzi yenye wanachama 69 ili achaguliwe moja kwa moja.
Hayya ni nani?
Chanzo cha picha, AP
Khalil al-Hayya (aliyezaliwa Novemba 5, 1960) ni mwanasiasa wa Palestina ambaye alihudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Ofisi ya Siasa ya Hamas hadi Agosti 2024.
Al-Hayya alipata shahada yake ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza, huku shahada yake ya uzamili ikitoka Chuo Kikuu cha Jordan.
Alipata Shahada yake ya Uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Holy Quran and Islamic Studies. Alijiunga na Hamas baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza. Wakati huo, alikuwa akifanya kazi kama mwalimu.
Al-Hayya alikuwa afisa wa Hamas kwa miongo kadhaa. Alichukuliwa kuwa mtu wa karibu wa kiongozi wa zamani wa Hamas, Yahya Sinwar, na alielezewa kama “mmoja wa watu wachache ambao Sinwar aliwaamini.”
Novemba 2019, al-Hayya na Rouhi Mushtaha waliongoza ujumbe ulioondoka Ukanda wa Gaza na kutembelea nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Uturuki na Lebanon.
Kabla ya safari hii, ujumbe huo unaripotiwa kukutana na maafisa wa ujasusi wa Misri mjini Cairo.
Al-Hayya pia aliongoza mazungumzo ya maridhiano na kundi la Fatah. Januari 2022, alitembelea Algeria, kufuatia mwaliko kutoka kwa rais wa Algeria.
Oktoba 2022, al-Hayya alitangaza kwamba yeye na wawakilishi wa makundi mengine ya Palestina walifanya mkutano wa “kihistoria” huko Damascus na Rais wa Syria Bashar al-Assad.
Al-Hayya alisema wakati huo kwamba wamekubaliana kukomesha mzozo kati ya Hamas na Syria, ambao ulianza wakati Hamas ilipokataa kuunga mkono utawala wa Bashar al-Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.
Al-Hayya aliiwakilisha Hamas wakati wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Israeli kuhusu kuachiliwa kwa mateka na wafungwa na kusitisha mapigano.
Ndugu saba hadi wanane wa al-Hayya, wakiwemo ndugu zake wawili, waliuawa katika mashambulizi ya Israel nyumbani kwake mwaka wa 2007.
Jaribio la kumuua limeshindwa. 2008, mmoja wa wanawe pia aliuawa katika shambulio la anga.
Mwana mwingine, mkwewe, na mjukuu waliuawa katika shambulio la anga nyumbani kwake Julai 2014 wakati wa vita vya Gaza vya mwaka huo.
Mustakbali wa Hamas
Chanzo cha picha, Reuters
Hamas inapitia moja ya vipindi vigumu zaidi katika historia yake.
Kundi hilo ambalo linatajwa kama shirika la kigaidi na Israeli, Uingereza, Marekani na nchi nyingine nyingi, limedhoofishwa sana na vita vya Gaza, viongozi wake wakuu wa kijeshi na kisiasa wameuawa, miundo yake ya utawala imeporomoka, na sehemu kubwa ya eneo la Palestina limeharibiwa.
Mchuano wa uongozi umefichua mgawanyiko mkubwa ndani ya Hamas kuhusu mustakabali wake.
Wafuasi wa Mesahaal wanasema Hamas inapaswa kujifunza kutokana na vita hivyo, kuachana na mkakati wa mapambano ya silaha, na kutumia mbinu ya kisiasa huku ikihifadhi malengo makuu ya harakati hiyo.
Hata hivyo, wafuasi wa Hayya wanasema viongozi wa Gaza, baada ya kubeba mzigo mkubwa wa mzozo huo, sasa wanapaswa kuongoza harakati hizo, hasa kuhusu suala la upokonywaji wa silaha.
Tangu Hamas ilipokubaliana makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel Oktoba iliyopita, Hamas kuweka chini silaha zake bila njia ya kisiasa kuelekea kujitawala kwa Palestina na kuwa taifa.
Imekataa mipango ya Bodi ya Amani inayoongozwa na Marekani ambayo inataka Hamas iweke silaha chini, kabla ya kuanza ujenzi mpya wa Gaza.
Hamas inalalamika kwamba kuna ukosefu wa dhamana ya usalama dhidi ya mashambulizi yanayoendelea ya Israeli na makundi yanayoibuka ya waasi wenye silaha.
Takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka katika shambulio la Hamas la mwaka 2023 dhidi ya Israel.
Israel ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi huko Gaza, ambapo zaidi ya watu 73,280 wameuawa, wakiwemo 1,158 tangu kusitishwa kwa mapigano, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoongozwa na Hamas.