KIGOMA: Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dk Rashidi Chuachua amewataka maofisa uvuvi kutumia nafasi zao kuchochea ajira kwa vijana kwenye sekta hiyo.
Dk. Chuachua amesema hayo akifunga mafunzo kwa wakaguzi na wasimamizi wa mazao ya uvuvi kutoka mikoa saba ya Tanzania Bara na Zanzibar yaliyoandaliwa ma Wizara ya Uvuvi kwa ufadhili wa Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Alisema kuwa bado mazao ya uvuvi yana soko kubwa ndani na nje ya nchi kutokana na mahitaji yaliyopo ambapo uzalishaji haujafika hata nusu ya mahitaji.
Alisema mahitaji ya mazao ya uvuvi kwa chakula ni makubwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu nchini lakini pia ongezeko la kibiashara nje ya nchi limeongezeka maradufu hivyo fursa ya ufugaji wa samaki ni kubwa fursa ambayo inaweza kutoa ajira kubwa kwa vijana.
Amewasisitiza maafisa uvuvi kutumia mafunzo hayo kwenda kusimamia ubora wa mazao yanayotokana na uvuvi ili yaweze kukidhi ubora na viwango vya soko la kimataiafa sambamba na kusimamia usalama na afya ya mazao ya uvuvi kwa watumiaji.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mratibu wa mradi wa kuboresha mnyororo wa thamani ya uvuvi na ufugaji samaki ili kuongeza kipato, kukuza uchumi, na kulinda mazingira (FISH4ACP) unaosimamia na FAO, Hashimu Muumin alisema kuwa sekta ya uvuvi ina nafasi kubwa ya kutengeneza ajira na kuongea shughuli za kiuchumi kwa watu mbalimbali.
Muumini alisema kuwa shughuli za uuvui haziishii ziwani au baharini pekee bali mchakato mzima wa mazao ya uvuvi unaishia hadi kwa mlaji wa mwisho ambapo watu mbalimbali kabla ya mazao ya uvuvi kumfikia mlaji wanakuwa wameingia kwenye ajira kwa kufanya shughuli mbalimbali.
Kwa upande wake Nankondo Senzira, Ofisa Uvuvi Mkuu anayeshughulikia Udhibiti wa Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko katika Wizara ya Uvuvi alisema kuwa mafunzo hayo tayakuwa na tija kubwa katika kutoa elimu na miongozo muhimu ya kuboresha biashara na masoko ya samaki na mazao mengine ya majini kwani kwa sasa wizara inasisitiza utekelezaji wa mikakati ya kibiashara katika mazao ya uvuvi.
