
“Kwa miongo kadhaa, ongezeko la haraka la shughuli za anga za juu limeonesha kila uzinduzi huacha athari kwa mazingira, na inaweza kuchukua muda mrefu kuelewa kikamilifu madhara yake. Ndiyo maana ni muhimu sana kuzingatia uendelevu wa programu hizi tangu mwanzo,” anasema Jason Jabbour, Afisa Mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP).
Kwa nini hili ni muhimu
- Taka za angani zinazozunguka dunia zinaongezeka kwa kasi.
- Uchafuzi unaotokana na satelaiti unaweza kuathiri angahewa na tabaka la ozoni.
- Mikataba ya Umoja wa Mataifa inahimiza uchunguzi wa anga unaowajibika na kupunguza taka za angani.
- Kulinda anga za juu kunasaidia kulinda maisha na mifumo ya ikolojia duniani.
Ingawa kuna makubaliano ya kimataifa ya kuzuia uchafuzi wa anga za juu, inakadiriwa kuwa vipande takriban milioni 140 vya taka za angani vyenye ukubwa wa zaidi ya milimita moja sasa vinazunguka dunia.
Vingi vya vipande hivyo ni vidogo mno kiasi kwamba haviwezi kufuatiliwa, lakini bado vina uwezo wa kuharibu satelaiti na vyombo vya angani.
Hata hivyo, wasiwasi wa kimazingira hauishii kwenye hatari ya migongano pekee.
Makundi ya satelaiti
Satelaiti zilizokoma kufanya kazi hatimaye huingia tena katika angahewa ya dunia, ambapo hutoa ‘metali’ kama vile alumini, lithiamu na shaba. Wanasayansi wanachunguza iwapo nyenzo hizi zinaweza kuathiri kemia ya angahewa, uundaji wa mawingu na tabaka la ozoni.
Sehemu za roketi zinazotenganishwa wakati wa uzinduzi pia huchangia tatizo hili. Baadhi hubaki angani kwa miaka mingi kabla ya kuvunjika au kuanguka tena duniani, huku nyingine zikisambaratika na kuwa maelfu ya vipande. Inakadiriwa kuwa mamia ya tani za vyombo vya angani na sehemu za roketi huingia tena katika angahewa kila mwaka, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kadiri makundi ya satelaiti yanavyozidi kuongezeka.
Vifaa vidogo vinavyohusiana na misheni za anga, ikiwemo bolti, vifuniko vya lenzi na vifuniko vya kinga, pia vinaongeza msongamano wa taka katika mzunguko wa dunia. Aidha, migongano na milipuko ya mara kwa mara huzalisha chembechembe ndogo ambazo wanasayansi wanaamini tayari zinaongeza mwangaza wa anga la usiku.
Hatari ya kudumu
Ingawa vyombo vingi vya angani huteketea vinaporejea katika angahewa ya dunia, baadhi ya vipande vikubwa vinavyostahimili joto vinaweza kufika ardhini, na hivyo kuhatarisha watu, miundombinu na viumbe wa baharini.
Kwa maelfu ya miaka, Mwezi umevutia wanadamu, ukichochea hadithi za kale, maendeleo ya sayansi na urambazaji, huku ukiendelea kuathiri maisha duniani kupitia nguvu zake za mvutano.
Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mwezi tarehe 20 Julai, Umoja wa Mataifa unaangazia si tu umuhimu wa jirani wa karibu zaidi wa dunia angani, bali pia changamoto za kimazingira zinazoambatana na enzi mpya ya uchunguzi wa anga.
Nafasi ya Mwezi katika kuendeleza maisha
Kutoka umbali wa karibu kilomita 400,000, Mwezi husababisha mawimbi ya bahari ambayo huongeza kiwango cha oksijeni katika maji ya pwani, husafirisha virutubisho na kusaidia kudumisha mifumo tajiri ya ikolojia ya baharini, ikiwemo Mwamba Mkuu wa Matumbawe. Wanasayansi wanasema kuuelewa Mwezi kunatoa maarifa muhimu kuhusu asili na maendeleo ya mfumo mzima wa Jua.
Katika miaka ya hivi karibuni, hamasa ya uchunguzi wa Mwezi imeongezeka kwa kasi. Mapema mwaka huu, misheni ya Artemis II ya NASA iliwapeleka wanaanga wanne katika safari ya siku 10 kuuzunguka Mwezi ikiwa sehemu ya mpango wa kuanzisha uwepo wa kudumu wa binadamu juu ya uso wa Mwezi katika miaka ya 2030. China, India, Japan na kampuni kadhaa binafsi pia zinaendeleza programu kabambe za uchunguzi wa Mwezi.
Lakini kadiri shughuli za anga zinavyoongezeka, ndivyo pia wasiwasi kuhusu athari zake kwa mazingira unavyoongezeka.
Dhana ya uendelevu wa anga inasisitiza kwamba uchunguzi na shughuli zote zinazofanyika nje ya dunia zinapaswa kulinda mazingira ya anga kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Msingi wa ulinzi
Kwa kuendeleza juhudi hizo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimepitisha mwongozo unaolenga kupunguza uundaji wa taka za angani kwa kupunguza mabaki yasiyo ya lazima, kuzuia milipuko, kuepuka uharibifu wa makusudi wa vyombo vya angani na kuondoa kwa usalama satelaiti na hatua za roketi zilizostaafishwa kutoka katika mzunguko wa dunia.
Chini ya Mkataba wa Uwajibikaji wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1972, nchi zinazozindua vyombo vya angani zinawajibika kwa uharibifu wowote unaosababishwa na vitu hivyo duniani, ikiwemo uzinduzi unaofanywa kwa ushirikiano wa nchi nyingi.
Ili kukabiliana na hatari hizi zinazoibuka, UNEP na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Anga za Juu, UNOOSA zinafanya kazi kwa pamoja kuimarisha uelewa wa kisayansi kuhusu athari za kimazingira za shughuli za anga na kuhakikisha kuwa ulinzi wa mazingira unajumuishwa katika mifumo ya baadaye ya usimamizi wa anga.
Kadiri binadamu wanavyojiandaa kwa kurejea kwa muda mrefu Mwezini, Umoja wa Mataifa unasema kuwa kulinda anga za juu na mazingira ya dunia lazima kubaki kuwa msingi wa hatua inayofuata ya uchunguzi wa anga.