Dar es Salaam. Rais wa Mpito wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore amezua mjadala baada ya kusema nchi hiyo haitaanzisha mfumo wa sheria za sharia, akisisitiza kila raia ana haki ya kufuata imani yake ya kidini.

Sharia ni mfumo wa sheria na kanuni za Kiislamu unaotokana na Qurani na Sunnah za Mtume Muhammad, unaoongoza ibada, maadili, familia na baadhi ya masuala ya kisheria.

Nchi zinazotumia sharia kwa viwango tofauti ni pamoja na Saudi Arabia, Iran, Afghanistan na Brunei. Afrika, inatambulika katika mifumo ya sheria ya nchi kama Mauritania, Somalia, Sudan na Nigeria hasa baadhi ya majimbo ya kaskazini.

Katika kauli hiyo, ambayo imeripotiwa na vyombo vya habari nchini humo kikiwemo Naijalamp na kuzua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, imeibua mjadala kuhusu nafasi ya dini, utawala na usalama wa taifa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi inayokabiliana na changamoto ya mashambulizi ya makundi yenye misimamo mikali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Juni 17, alipozungumza na viongozi wa makundi mbalimbali na dini kaskazini mwa nchi hiyo, Traore alisema licha ya yeye kuwa Mwislamu, Burkina Faso itaendelea kuwa nchi inayoheshimu uhuru wa wananchi wake kuchagua na kutekeleza imani zao.

“Mimi ni Muislamu, lakini kila mtu nchini Burkina Faso ana haki ya kufuata dini yake. Hakutakuwa na Sharia katika nchi hii,” alinukuliwa Traore katika hotuba yake iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Katika maelezo yake, rais huyo wa mpito pia alizungumzia suala la baadhi ya raia wa Burkina Faso wanaosoma masomo yanayohusiana na sharia nchi za nje ikiwemo Saudi Arabia, akiwataka kuzingatia zaidi ujuzi wa kiteknolojia na taaluma zinazoweza kuchangia maendeleo ya nchi.

“Wanafunzi wanaokwenda nje ya nchi wanapaswa kutafuta maarifa yatakayosaidia kujenga uchumi na uwezo wa kitaifa badala ya kujikita kwenye masomo ambayo hayatoi mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya taifa,” amenukuliwa Rais Traole.

Kauli hiyo imekuja wakati Burkina Faso ikiendelea kupambana na makundi yenye silaha yanayohusishwa na itikadi kali za kidini, hali ambayo imeathiri usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Tangu alipoingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2022, Traore ameibuka kuwa rais kijana maarufu zaidi, akisisitiza ajenda ya kujenga taifa lenye kujitegemea, kuimarisha usalama na kupunguza utegemezi wa mataifa ya kigeni.

Hata hivyo, kauli yake kuhusu wanafunzi wa sharia nchini Saudi Arabia imepokea maoni tofauti kutoka kwa watu mbalimbali nchini humo.

Baadhi ya wafuasi wake wamepongeza msimamo huo wakisema unalenga kuzuia matumizi mabaya ya dini katika siasa na kulinda umoja wa kitaifa wakati

Wakosoaji wake wakihoji iwapo msimamo huo unaweza kuathiri uhuru wa elimu na haki ya watu kusoma taaluma zinazohusiana na dini.

Mjadala huo unaendelea katika kipindi ambacho mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi yanakabiliwa na changamoto ya makundi yenye silaha yanayotumia misingi ya kidini kuhalalisha vitendo vya vurugu.

Burkina Faso, pamoja na nchi jirani katika eneo la Sahel zikiwemo Mali na Niger, zimeendelea kukumbwa na mashambulizi ya makundi yenye uhusiano na mitandao ya kigaidi ya kimataifa.

Aidha, serikali ya Traore imeendelea kusisitiza kuwa kipaumbele chake kikubwa ni kurejesha usalama, kuimarisha uchumi na kujenga uwezo wa ndani wa Burkina Faso kupitia elimu, teknolojia na uzalishaji wa ndani tofauti na misaada na wafadhili kutoka mataifa ya magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *