
Afisa wa shirika hilo Valentine Naserian anafafanua akisema, “tunahifadhi mazingira kwa kufuga nyuki. Nyuki imetusaidia sana kwa kuhifadhi mazingira kwa sababu kila mtu anajua nyuki anapenda mazingira ya kwanza imetulia mazingira safi na pia inapenda miti na maua.”
Ignite 254 na usaidizi
Lekurruki katika shughuli hizi hushirikiana na wadau. Miongoni mwao ni Mapenzi Baya kutoka shirika la Ingnite Two Five Four. Bi. Baya baada ya kukagua maendeleo ya miradi ameelezea kile wanachowasaidia kuwa ni pamoja na mafunzo ya ufugaji nyuki na mbinu za kuvuna asali. Na zaidi ya hapo ni uwezeshaji vijana kiuchumi.
“Na hii tumeona ni kitu ambacho wanaweza fanya kujikuza kimaisha. Wanaweza kupata asali na kuuza na kupata kipato. Pia ni shughuli ambayo haichukui muda mwingi sana. Hiki ni kitu unafanya huku ukiendelea na shughuli nyingine. Kwa hivyo ningeweza kuwaambia vijana kuwa ni shughuli ambayo wanafaa kuwa wakijishughulisha nayo.”
Ufugaji nyuki unatumia gharama kidogo
Bi. Baya anawasihi vijana kuchangamkia ufugaji wa nyuki, akisema gharama ya ufugaji nyuki ni kidogo sana. Anasema, “kama kuna mahali unaweza akalima mimea kadhaa kadhaa na unaweza pia weka mzinga wa nyuki itakuwa ni muhimu sana. Halafu pia ile mimea ambayo unaweka pale inakuwa ni ile inasaidia kwa uzalishaji wa hii asali.”
Akaenda mbali zaidi kufafanua kuwa Lekurruki hutoa mafunzo kwa wale ambao bado hawajaingia katika programu ya ufugaji wa nyuki, sambamba na mikakati ya kutafuta masoko . Anasema, “Kuna wale ambao wanataka hiyo nafasi ya kufunzwa pia nao wanawafunza ningependa wawasiliane nao. Wataweza kufuzu, wataweza kukaribishwa kwa haya mafunzo”
Uhakika wa kupata chakula
Kando ya ufugaji wa nyuki, kuna mradi wa kuhakikisha wanajamii wana uhakika wa kupata chakula, ikiwa ni kutelekeza lengo namba 2 la kutokomeza njaa. Lekurruki inatekeleza hilo kwa kuanzisha bustani za vyakula na mboga.
Bi. Naserian anasema wamepanda mazao kama vile mihogo na pia, “Tumepanda mboga kama spinach. Tumepanda cabbage, tumepanda viazi na mboga hizo zote ni za kienyeji na zinasaidia kwenye damu.”
Anasema lengo ni kuhakikisha upatikanaji wa mboga kwa jamii na kisha wauze kilo moja shilingi 20 za Kenya, sawa na dola senti 15.
“Tunataka tuwe na mboga nyingi ili wanakijiji wasikose mboga na hivyo tumalize shida ya ukosefu wa chakula.”
Vijana changamkieni fursa
Bi. Naserian anatamatisha kwa kuwataka vijana kuondoka katika maeneo yao ya faraja na kuacha kudai kuwa hakuna kazi, akisisitiza kuwa fursa za ajira na kujipatia kipato zipo nyingi kwa wale walio tayari kuzitafuta na kuzitumia akitolea mfano ufugaji wa nyuki.
“ Nyuki hauhitaji wewe kuweko hapo kila wakati. Muhimu ni mazingira na upande miti na kuweko na maji. Kama eneo la Ngong na eneo letu hapa nyuki wanapenda kwa kuwa kuna miti na maua. Usikae ndani tu, toka nje hakuna kitu kitakufuata kwenye kiti.”