Songwe. Mwanafunzi wa darasa la saba, Simoni Mwamlima (15), ameuawa katika tukio lililotokea Kitongoji cha Chang’ombe, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe, huku Jeshi la Polisi likiendelea na msako wa kuwabaini na kuwakamata watu wanaohusishwa na mauaji hayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Julai 20, 2026, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, Simoni, aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Ntungwa, alikutwa akiwa na jeraha la kukatwa kwa kitu chenye ncha kali nyuma ya shingo.

Kamanda Senga amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Simoni aliondoka nyumbani kwao Julai 17, 2026, saa 2:00 usiku, akielekea dukani kununua betri za tochi, lakini hakurejea hadi mwili wake ulipopatikana siku iliyofuata.

Amesema tukio hilo ni miongoni mwa matukio mawili ya mauaji yaliyotokea katika wilaya za Momba na Mbozi, ambayo Jeshi la Polisi linaendelea kuyafanyia uchunguzi.

“Katika tukio la pili, lililotokea Julai 19, 2026, saa 7:30 mchana, katika Kitongoji cha Nzije A, Kata ya Halungu, Wilaya ya Mbozi, George Songa (55) aliuawa akiwa ndani ya nyumba yake baada ya kushambuliwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kwenye mkono wa kulia,” amesema.

Kamanda Senga amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo, sambamba na msako wa kuwabaini na kuwakamata wahusika ili wafikishwe mahakamani.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea na uchunguzi wa matukio haya huku likiwasaka watuhumiwa. Tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana nasi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini na kuwakamata wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria,” amesema Kamanda Senga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *