Dar es Salaam. Serikali ya Marekani imefafanua mfumo wake wa tahadhari za safari za kimataifa, ikieleza viwango vinne vinavyotumika kutathmini mazingira ya usalama katika nchi mbalimbali duniani, huku mataifa 23 yakiwekwa kwenye kiwango cha juu zaidi cha tahadhari.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, mfumo huo unalenga kuwasaidia raia wake kufanya uamuzi kuhusu safari zao kwa kuzingatia hatari zinazoweza kujitokeza katika maeneo wanayokwenda.

Katika waraka huo, wizara hiyo ilisema jukumu lake kuu ni kuhakikisha usalama wa raia wake walioko nje ya nchi, ikisisitiza kuwa tahadhari hizo hazimaanishi kupima usalama wa wananchi wa mataifa husika, bali kutathmini mazingira yanayoweza kuwaathiri raia wa Marekani.

“Hakuna jambo lenye kipaumbele kikubwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuliko usalama na ulinzi wa raia wake walioko nje ya nchi,” inaeleza taarifa hiyo.

Mfumo huo umegawanywa katika viwango vinne. Kiwango cha kwanza kinashauri wasafiri kuchukua tahadhari za kawaida kwa kuwa ndicho kiwango cha chini zaidi cha hatari.

Kiwango cha pili kinawataka kuongeza umakini kutokana na uwepo wa hatari zilizoongezeka.

Kiwango cha tatu kinashauri wasafiri kufikiria upya mipango yao ya safari kutokana na uwepo wa hatari kubwa, huku kiwango cha nne, kinachoitwa ‘Usisafiri,’ kikiwa ndicho cha juu zaidi, ambapo Marekani inaeleza kuwa inaweza kuwa na uwezo mdogo au kutokuwa na uwezo kabisa wa kutoa msaada wakati wa dharura.

Marekani inaeleza kuwa nchi huwekwa katika viwango hivyo baada ya kuchunguza mambo mbalimbali, ikiwamo uhalifu, ugaidi, machafuko ya kisiasa, changamoto za afya, majanga ya asili, utekaji nyara na kuzuiliwa kinyume cha sheria.

Katika masuala ya usalama, tathmini huzingatia uwepo wa vitisho maalumu au mashambulizi yanayoweza kuwaweka raia wake katika hatari, huku eneo la afya likitathmini uwezo wa huduma za tiba, hospitali, wataalamu na huduma za dharura katika nchi husika.

Nchi 23 zawekwa kiwango cha juu

Mataifa 23 yaliyowekwa katika kiwango cha nne cha tahadhari yanatoka katika mabara mbalimbali, huku Afrika ikiwa na idadi kubwa zaidi.

Nchi za Afrika zilizotajwa ni Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya, Mali, Niger, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda.

Katika bara la Asia zimetajwa Afghanistan, Myanmar, Iran, Iraq, Lebanon, Korea Kaskazini, Syria na Yemen. Ulaya zimetajwa Belarus, Urusi na Ukraine, huku Haiti ikiwa nchi pekee kutoka eneo la Karibea.

Marekani inaeleza kuwa viwango hivyo hupitiwa mara kwa mara kulingana na mabadiliko ya hali ya usalama, na viwango vya tatu na vya nne vinaweza kufanyiwa mapitio angalau kila baada ya miezi sita au wakati wowote kunapotokea mabadiliko makubwa.

Hatua hiyo si mpya katika mwenendo wa sera za Marekani kuhusu usalama na uhamiaji. Tangu mwishoni mwa mwaka 2025, Serikali hiyo ilianza kuongeza ukaguzi katika baadhi ya taratibu za uhamiaji.

Desemba 4, 2025, Marekani ilisitisha baadhi ya maombi ya uhamiaji kutoka mataifa 19 na kuagiza waombaji hao kufanyiwa uchunguzi zaidi, ikiwamo mapitio mapya ya maombi na mahojiano ya ziada.

Wakosoaji wa hatua hizo walieleza kuwa sera hizo zinaweza kuwaathiri wahamiaji wasiokuwa na makosa kwa kuwafanya raia kutoka baadhi ya mataifa waonekane kuwa na mashaka kabla ya tathmini binafsi kufanyika.

Athari kwa diplomasia na uchumi

Wataalamu wa masuala ya kimataifa na uchumi wanaeleza kuwa tahadhari hizo zinaweza kuathiri zaidi ya masuala ya usalama, ikiwamo taswira ya nchi, biashara, uwekezaji na utalii.

Mtaalamu wa diplomasia ya uchumi, Profesa Kitojo Wetengere, anasema ukubwa wa uchumi wa Marekani duniani unafanya hatua zake kuwa na uzito kwa mataifa yanayoshirikiana nayo.

“Ukubwa wa Marekani kiuchumi pia una mchango mkubwa, hivyo kikwazo chake lazima mataifa yataathirika kwa namna moja ama nyingine,” anasema.

Anasema nchi zinapaswa kutumia njia za kidiplomasia kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza na kujenga mahusiano mapana na washirika wengine wa kimataifa ili kupunguza athari.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Denis Konga, anasema tahadhari hizo zinaweza kuathiri mtazamo wa kimataifa kuhusu nchi zinazotajwa, hasa zinapohusishwa na masuala ya usalama.

Anasema ni muhimu nchi kutumia diplomasia ya mawasiliano kueleza hali halisi ya mazingira yao ili kuzuia tahadhari hizo pekee kujenga taswira hasi kimataifa.

Kwa upande wa uchumi, wataalamu wanaeleza kuwa wawekezaji na wasafiri wa kimataifa huzingatia viashiria vya usalama kabla ya kufanya maamuzi. Hivyo, tahadhari za kiwango cha juu zinaweza kuathiri mtiririko wa watu, mitaji na shughuli za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *