Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuiondoa Kigoma katika historia ya kuwa mwisho wa reli na kuigeuza kuwa kitovu cha biashara, usafirishaji na uwekezaji kinachounganisha Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Amesema hatua hiyo inatekelezwa kupitia uwekezaji wa Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa Bandari ya Kigoma na ujenzi wa meli za mizigo katika Ziwa Tanganyika, miradi inayolenga kufungua fursa mpya za uchumi kwa wananchi.

Rais Samia, ameyasema hayo leo Jumatatu, Julai 20, 2026 wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa SGR kipande cha Tabora-Kigoma na uzinduzi wa ujenzi wa meli nne za mizigo mkoani Kigoma.

Amesema tangu alipotembelea Kigoma mwaka 2022 aliahidi kuufungua mkoa huo kiuchumi kwa kutumia nafasi yake ya kijiografia na kwamba miradi inayotekelezwa sasa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi hiyo.

“Niliahidi Kigoma haitakuwa mwisho wa reli tena. Itakuwa katikati kutoka Dar es Salaam kwenda mbele na kila tunachokifanya leo ni utekelezaji wa ahadi hiyo,” amesema.

Amesema Kigoma ina nafasi muhimu kwa sababu ni lango la Tanzania kuelekea nchi jirani, hivyo maendeleo ya reli, bandari na usafiri wa majini yataifanya kuwa kitovu cha biashara za kikanda.

“Kigoma haitakuwa mwisho wa reli kama ilivyozoeleka kufahamika, bali mwanzo wa kufunguka kwa fursa za biashara na uwekezaji,” amesema.

Baadhi wananchi waliohudhuria katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha sita kutoka Tabora-Kigoma kwenye hafla iliyofanyika leo Julai 20, 2026 Katosho mkoani Kigoma.

Mkuu huyo wa nchi, amesema reli hiyo itakapokamilika itaunganisha Kigoma na Tabora, Dodoma, Morogoro hadi Dar es Salaam, huku ikiunganishwa na mtandao mpana wa reli unaoelekea Mwanza.

Amesema hali hiyo itarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Kigoma na kurahisisha bidhaa kutoka Kigoma kufika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa wakulima watanufaika kwa kupata pembejeo kwa urahisi na gharama nafuu, huku mazao yao yakifikishwa sokoni kwa haraka zaidi kuliko ilivyo sasa.

Pia, amesema wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara watanufaika kutokana na kupungua kwa gharama za usafirishaji na kuongezeka kwa fursa za masoko.

“Tujiandae na kuchangamkia fursa hizi. Uwekezaji huu ni kwa faida ya wana Kigoma na unakwenda kustawisha maisha yao,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Sita kutoka Tabora-Kigoma kwenye hafla iliyofanyika leo Julai 20, 2026 Katosho mkoani Kigoma.

Mbali na reli, Rais Samia amesema ujenzi wa meli nne za mizigo katika Ziwa Tanganyika utapanua uwezo wa usafirishaji kati ya Tanzania, Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwaka 2024, Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 61.5 (takriban Sh162.15 bilioni) kwenda Burundi.

Bidhaa kuu zilizouzwa ni pamoja na saruji, mbolea, chuma na bidhaa za chuma, mafuta ya petroli, nafaka, bidhaa za viwandani na vipodozi.

Kwa upande mwingine, Tanzania iliagiza bidhaa kutoka Burundi zenye thamani ya karibu dola za Marekani 996,540 (takriban Sh2.63 bilioni) mwaka 2024. Bidhaa hizo ni pamoja na kahawa, chai, magari, sabuni na baadhi ya bidhaa za viwandani.

Aidha, mwaka huohuo, Tanzania iliuza bidhaa kwenda DRC zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 313.3 (takriban Sh825.9 bilioni).

DRC ilikuwa soko la nane kwa ukubwa kwa bidhaa za Tanzania, ikichukua takribani asilimia 3.6 ya mauzo yote ya Tanzania nje ya nchi.

Rais Samia, amesema uwekezaji huo utavutia kampuni zaidi za usafirishaji, vituo vya kuhifadhi mizigo na shughuli nyingine za lojistiki zitakazochochea ukuaji wa uchumi wa Kigoma.

Kuhusu amani, ulinzi miundombinu

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia amesisitiza amani, usalama na maendeleo ya nchi, akidokeza uwekezaji huo umegharimu fedha nyingi na wananchi wana wajibu wa kikatiba na kizalendo kulinda miundombinu yote.

“Hujuma yoyote dhidi ya miundombinu hii si hasara kwa Serikali peke yake, bali kwa kila Mtanzania, kila anayelipa kodi na nchi kwa ujumla. Lakini sio tu kwa sisi tuliopo hata kizazi kijacho,” amesema.

Amesema fedha inayowekezwa ikiharibiwa itakuwa vigumu kupata kiasi hicho na kurudisha mradi, hivyo hilo litafifisha maendeleo ya kizazi kijacho.

“Niwaombe wananchi wa Kigoma wote kuwa na itikadi ya usalama kwanza kisha maendeleo. Kusingekuwa na usalama tusingeweka jiwe la msingi hapa, wana Kigoma msingefurika kwa wingi hapa kila mtu angekuwa amejifungia na kuogopa kutoka,” amesema.

Amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuweka mikakati madhubuti na shirikisho ya ulinzi wa miundombinu inayojengwa, kwani suala la usalama ni kipaumbele na halipaswi kupuuziwa.

“Tusikubali kushawishiwa au kutumika na watu wasioitakia mema nchi yetu, wawe wa ndani au nje ya nchi yetu. Tukivuruga amani na usalama wa nchi yetu maendeleo haya tunayoyataka hayatashamiri na hayatakuwa na maana,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Sita kutoka Tabora-Kigoma, baada ya kuwasili Katosho mkoani Kigoma.

Ameijenga hoja hiyo akitolea mfano baadhi ya nchi jirani, licha ya kuwa na ardhi lakini wanashindwa kulima na kupata chakula cha kujitegemea kwa sababu ya kukosa amani na usalama.

“Sote tuwe macho na tuepuke wasaliti na maadui wa nchi yetu,” amesema Rais Samia.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema uwekezaji wa meli nne za mizigo unaonyesha jinsi mazingira yaliyowekwa na Serikali yalivyowezesha sekta binafsi kuwekeza katika miradi mikubwa ya uchukuzi.

Amesema meli hizo zitafungua enzi mpya ya usafirishaji wa majini katika Ziwa Tanganyika na kuimarisha biashara kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kati.

“Uwekezaji huu unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 600 za moja kwa moja kwa wakazi wa Kigoma na kuchochea biashara nyingine zinazotegemea sekta ya usafirishaji,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Zijing Mining Group, Shaoyang Shen amesema maboresho ya Bandari ya Kigoma yataimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Mradi huu utaongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, ikiwemo madini yanayosafirishwa kutoka Kalemie nchini Congo kuelekea Bandari ya Dar es Salaam na masoko ya kimataifa,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro, amesema mradi wa SGR utaunganisha mkoa huo na Dar es Salaam na kupunguza muda wa usafirishaji wa mizigo na abiria.

Sirro ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu amesema reli hiyo itaongeza ushindani wa biashara, kuvutia uwekezaji wa viwanda na kufungua masoko mapya kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.

Sirro, amesema meli mpya zitasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa usafiri wa mizigo katika Ziwa Tanganyika, ambayo kwa sasa huchelewesha biashara za nchi jirani.

“Wakati mwingine wafanyabiashara hulazimika kusubiri zaidi ya mwezi mmoja kabla mizigo yao haijasafirishwa kwenda Kalemie,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *