
Na ni katika muktadha huo, kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na kikao cha wazi cha kupata taarifa na kufanya mashauriano ya faragha kuhusu taifa hilo ambako kikosi kipya kinachoungwa mkono na UN (GSF), ili kukabiliana na magenge ya uhalifu kimeanza kazi mwezi Juni mwaka huu.
Fahamu kuhusu GSF
Kutoka Barazani
Carlos Ruiz Massieu, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeongoza Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuweka utulivu nchini Haiti ( BINUH ) amesisitiza umuhimu wa uratibu wa karibu kati ya ofisi yake, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Usaidizi kwa Haiti, (UNSOH), GSF, taasisi za Haiti na washirika wa kimataifa.
“Mafanikio yanategemea usalama, ushiriki wa kisiasa na hatua za kibinadamu kuimarishana kwa pamoja,” amesema.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa operesheni za usalama pekee haziwezi kuleta amani ya kudumu na kwamba, “kufanikisha hilo kutahitaji mkakati mpana zaidi—mkakati unaopunguza ushawishi na uwezo wa magenge yenye silaha, unaoimarisha mfumo wa haki na taasisi za serikali, na unaotengeneza fursa kwa jamii zilizoathiriwa na vurugu, hususan wanawake na watoto.
Fahamu kuhusu vitisho kutoka magenge yaliyojihami hapa.
Magenge yenye silaha nchini Haiti hayalengi tena tu kuteka maeneo, amesema Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Monica Juma.
Magenge ya uhalifu sasa yanataka kuteka mifumo ya utawala
Akizungumza baada ya ziara yake nchini humo wiki iliyopita, ameliambia Baraza la Usalama kuwa magenge hayo “hayatafuti tena tu kudhibiti maeneo, bali yanataka kuteka mifumo ya utawala na nguzo za shughuli za kiuchumi ambazo jamii na taasisi zinategemea.”
Ameongeza kuwa magenge yanataka kudhibiti “njia kuu za usafirishaji, usambazaji wa mafuta na mitandao ya usambazaji wa chakula.”
Bi. Juma ameeleza kuwa uhalifu wa kupangwa unaendelea kubadilika, na katika baadhi ya maeneo kuchukua nafasi ya mamlaka ya dola, hali ambayo kimsingi imeifanya serikali na wananchi kuwa mateka.
Ameeleza kuwa hali hiyo ni “mgogoro wa utawala unaochochewa na uhalifu wa kupangwa, wenye athari kwa uchaguzi ujao, mwitikio wa kibinadamu na ustawi wa muda mrefu wa nchi.”
Takwimu nyuma ya mjadala wa leo kuhusu maisha ya watu
- Watu milioni 6.4 wanahitaji msaada wa kibinadamu.
- Takribani watu milioni 1.5 wamelazimika kuyahama makazi yao, nusu yao wakiwa watoto.
- Zaidi ya watu milioni 5.8 wanatarajiwa kukabiliwa na njaa kali mwaka huu.
- Mashirika ya kibinadamu yanaonya kuwa fedha za kufadhili shughuli zao zinaendelea kuisha wakati mahitaji ya msaada yanaendelea kuongezeka.
Haiti yataka ‘kutambuliwa kwa maendeleo yake’
Fursa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Haiti, Raina Forbin, ilipowadia, aliitumia kutoa ujumbe wa matumaini kwa kulieleza Baraza la Usalama kuwa nchi yake iko karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kurejesha usalama na kufanya uchaguzi huru.
“Tangu Januari mwaka huu, serikali ya Haiti imewafundisha zaidi ya askari wapya 2,000 wa polisi. Uandikishaji wa wapiga kura unaendelea, huku mikoa saba kati ya kumi ikiwa tayari kwa ajili ya uchaguzi,” amesema Waziri huyo.
Bi. Forbin amesema kuwa mamlaka za mitaa pia zinaandaa mipango ya kuwajumuisha tena katika jamii waliokuwa wanachama wa magenge ya uhalifu, pamoja na kutekeleza mageuzi ya mfumo wa haki na kuanzisha mahakama maalumu za kushughulikia makosa yanayohusiana na magenge hayo.
“Kwa muda mrefu sana, Haiti imekuwa ikitambulishwa kupitia migogoro yake,” amesema. “Leo, Haiti inataka kutambuliwa kwa maendeleo ambayo imeyapiga.”