Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent imepanda na kuvuka dola 90 kwa pipa kutoka kiwango cha takribani dola 70 ilichokuwa imefikia baada ya makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Marekani, huku matumaini ya dunia ya kuona bei za mafuta zikishuka yakizidi kuyeyuka baada ya Iran kutangaza kuzilipua meli nyingine mbili za mafuta zilizokuwa zikijaribu kuvuka Mlango wa Hormuz ambapo tukio hilo limezidisha hofu ya kuvurugika kwa usafirishaji wa mafuta kupitia njia hiyo muhimu ya kimataifa na kuongeza presha katika soko la nishati duniani.
Kupanda kwa bei ya mafuta kunatajwa kuwa pigo jipya kwa uchumi wa dunia kutokana na mafuta kuwa mhimili wa shughuli nyingi za kiuchumi huku wachambuzi wakisema ongezeko hilo linasababisha kuongeza gharama za usafiri wa anga, baharini na barabarani, uzalishaji viwandani, kilimo, ujenzi, uchimbaji madini na usafirishaji wa bidhaa, hali inayoweza kuchochea mfumuko wa bei, kuongeza gharama za maisha na kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi katika mataifa mengi yanayotegemea uagizaji wa mafuta.
Kwa mujibu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC), meli hizo mbili zililipuliwa katika njia ya kusini ya Mlango wa Hormuz, huku Iran ikidai zilikuwa zimekiuka taratibu zake za usafiri.
Mlango wa Hormuz hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani kwa njia ya bahari, hivyo tukio lolote la kiusalama katika eneo hilo huathiri moja kwa moja upatikanaji wa mafuta na mwenendo wa bei katika soko la dunia. Hali inayoongeza taharuki kwa kampuni za usafirishaji wa mafuta, kampuni za bima na masoko ya fedha.
Wataalamu wa sekta ya nishati wanaonya kuwa endapo mivutano kati ya Iran na Marekani itaendelea, upatikanaji wa mafuta unaweza kupungua zaidi na bei ya Brent kuendelea kupanda katika siku zijazo.
Kwa nchi zinazoagiza mafuta kutoka nje, hali hiyo inaweza kuongeza matumizi ya fedha za kigeni, kupandisha gharama za uzalishaji na usafirishaji, kuongeza bei za bidhaa na huduma pamoja na kuathiri juhudi za mataifa mengi kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha uchumi.

(Feed generated with FetchRSS)