
KIUNGO wa kimataifa wa Guinea, Naby Camara huenda akarejea tena katika klabu ya Al Waab inayoshiriki Ligi Daraja la Pili maarufu Qatari Second Division baada ya kupewa mkono wa kwaheri na Simba.
Kabla ya kutua Simba msimu uliopita nyota huyo aliwahi kuitumikia Al-Waab msimu wa 2024/25 akiwa mchezaji muhimu kikosini.
Habari ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa watu wa karibu na mchezaji huyo zinaeleza kuwa pamoja na Al-Waab kuonyesha nia kubwa ya kumrejesha, kuna timu mbili za Ligi Kuu ya Qatar zinamfuatilia na zimeanza mazungumzo naye.
Tofauti na klabu hizo mbili, inaelezwa Waab iko karibu kukamilisha usajili huo kutokana na kumfahamu vizuri Camara na kiwango alichokionyesha alipokuwa akiitumikia Waab kabla ya kuhamia Simba.
“Wamekuwa na mazungumzo kwa muda mrefu na bado hakuna timu iliyofikia makubaliano lakini Waab wamekuwa na uhitaji mkubwa zaidi na kiungo kwa hiyo lolote linaweza kutokea,” amesema mmoja wa watu wa karibu wa kiungo huyo.
Camara ameondoka Simba baada ya kutokuwa sehemu ya mipango ya kikosi cha kocha Steve Barker kuelekea msimu mpya, hatua iliyomfanya aanze kutafuta changamoto nyingine nje ya Tanzania.
Kutokana na uzoefu wake katika soka la Tunisia alipoiichezea CS Sfaxien, Qatar na timu ya taifa ya Guinea, Camara mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani huenda akawa mmoja wa nyota watakaounda kikosi hicho msimu ujao.
Kiungo huyo alisajiliwa wakati wa kocha Fadlu Davids na alikuwa akipata nafasi ya kuanza mara kwa mara lakini tangu Steve Barker alipochukua mikoba Camara hakuwa na nafasi ya kucheza.
Akiwa na Simba Camara amecheza mechi 11 za mashindano hayo, tano za Ligi Kuu, moja ya ngao ya jamii na tano za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.