MABINGWA wa Ligi Kuu Bara Yanga imefanya mazungumzo ya mkataba mpya na kipa wake mzawa, Hussein Masalanga na kufikia makubaliano ya kumuongezea mwaka mmoja utakaoisha mwakani.

Januari 18, 2026, Yanga ilimsajili Masalanga kutoka Singida Black Stars na mkataba wake ulipoisha baada ya ligi kumalizika, uongozi wa klabu hiyo umeona huduma yake bado inaendelea kuhitajika.

Chanzo cha ndani kutoka Yanga, kilisema tayari Masalanga amesaini  mkataba wa mwaka mmoja ni mambo machache yamesalia ili kukamilisha kila kitu.

“Masalanga ni miongoni mwa makipa wazawa wenye uwezo mzuri ndiyo maana amekuwa akiitwa timu ya taifa, hivyo tumeona tunahitaji kuendelea naye kwa ajili ya msimu unaoanza Agosti 14, 2026,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Ukiachana na Masalanga kuna wachezaji wengine ambao walikuwa wamemaliza mikataba, tutazungumza nao kwa ajili ya kuwaongezea kama nahodha Bakari Mwamnyeto, Kibwana Shomari na wengine wengi pia ambaye tulishamuongezea ni  Kouassi Yao.”

Hata hivyo, pamoja na mkataba huo, bado kipa huyo atatakiwa kufanya kazi ya ziada kama anataka kupata namba kwenye timu hiyo kutokana na uwepo wa Djigui Diarra ambaye amekuwa na kiwango bora kwenye timu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *