
Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi (UNHCR) umetangaza kuwawatu 144 wameripotiwa kufariki au kutoweka katika pwani ya Mauritania walipokuwa wakijaribu kufika Ulaya.
Katika taarifa leo Jumanne, UNHCR imesema idadi hiyo imekuja baada ya operesheni tatu za uokoaji zilizofanyika Mauritania kati ya Julai 14 hadi 18. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kupanuliwa kwa fursa za elimu na ajira barani Afrika ili kuwazui vijana kuhatarisha maisha yao katika safari hatari za kuvuka bahari kuelekea Ulaya..
Kwa mujibu wa UNHCR, jumla ya watu 143 walifariki ndani ya chombo kimoja cha majini kilichoondoka Bufaloto, Gambia, na kuokolewa tarehe 18 Julai baada ya kukwama baharini kwa muda wa siku 25.
Msemaji wa shirika hilo, Matt Saltmarsh, aliambia mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva kwamba:
“Miongoni mwa manusura wa chombo hicho walikuwemo watoto wawili ambao wamepoteza wanafamilia wao wote katika safari hiyo, na kwa sasa wanapatiwa matibabu hospitalini.”
Amesema waathiriwa hao walitoka katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, bila kutoa maelezo zaidi.
Shirika hilo limeongeza kuwa, kwa ujumla, operesheni tatu za uokoaji zilizofanyika kati ya Julai 14 hadi 18 nchini Mauritania zilisababisha watu 387 kuokolewa
Mpaka sasa katika mwaka 2026, jumla ya kutua kwa vyombo 17 vya usafiri baharini kumerekodiwa katika miji ya Nouadhibou na Nouakchott nchini Mauritania, ambapo watu 2,147 wameokolewa kwa jumla.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa idadi ya wahamiaji na wakimbizi wanaowasili Ulaya kwa njia ya bahari kupitia njia kuu imepungua kwa zaidi ya theluthi moja mwaka huu, huku idadi hiyo ikiwa ni zaidi kidogo ya 40,000, ikilinganishwa na 65,407 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025.
Hata hivyo, UNHCR imesisitiza kuwa licha ya kupungua kwa idadi ya wanaowasili, kiwango cha vifo na watu kutoweka bado kipo katika hali ya kutisha sana.