Arusha. Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), ameshindwa katika juhudi zake za kuiomba Mahakama Kuu ibadilishe hukumu ya miaka mitatu jela dhidi ya Kenes  Mbukwa, aliyekutwa na dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 100.

Mahakama Kuu Masjala Ndogo wa Mbeya, imesema kuwa DPP hakuweka msingi wa kisheria wa kuiwezesha Mahakama hiyo kubadili kosa kukutwa na dawa hizo za kulevya ambalo Mbukwa alikutwa nalo na kumtia hatiani kwa kosa jingine la usafirishaji haramu wa dawa za kulevya.

Uamuzi huo umetolewa Julai 20,2026 na Jaji Musa Pomo katika rufaa ya jinai namba 20770/2025,iliyokatwa na DPP kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya katika Kesi ya jinai namba 35413/2024.

Kwa uamuzi huo, Mahakama Kuu imetupilia mbali rufaa ya DPP na kuacha hukumu ya kifungo cha miaka mitatu jela iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ikiwa imesimama.

Chanzo cha kesi

Mbukwa alikamatwa Desemba 13, 2024, katika eneo la Iyanga, Kata ya Ilomba,mkoani Mbeya, akiwa na dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 100.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano pamoja na vielelezo mbalimbali, ikiwemo misokoto 84 ya bangi, nyaraka za ukamataji, maelezo ya onyo pamoja na simu ya mkononi.

Ushahidi wa upande wa mashtaka ulidai kuwa maafisa wa Polisi na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) walifanya operesheni baada ya kupata taarifa kuwa Mbukwa alikuwa akijihusisha na biashara ya bangi.

Mbukwa alikamatwa na kupekuliwa mbele ya viongozi wa eneo hilo, ambapo misokoto 84 ya bangi na simu ya mkononi aina ya Tecno vilidaiwa kupatikana kutoka kwake.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mahakama ya Wilaya ya Mbeya ilimkuta Mbukwa na hatia ya kumiliki dawa za kulevya kinyume cha sheria chini ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela.

Rufaa ya DPP

Katika rufaa hiyo DPP aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Upendo Lyimo huku mjibu rufaa akiwa hana uwakilishi wa wakili.

DPP alikuwa na hoja moja kuwa hakimu alifanya makosa kisheria kwa kutoa hukumu ambayo haifai kwa mujibu wa sheria na kudai kuwa Mahakama ilijielekeza vibaya katika kumtia hatiani mjibu maombi kwa kumiliki dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 17 cha sheria tajwa juu.

Alidai kuwa Mahakama ya Wilaya ilikosea kisheria kwa kumtia Mbukwa hatiani kwa kosa la kumiliki dawa za kulevya badala ya kosa la usafirishaji haramu wa dawa za kulevya chini ya kifungu cha 15A(1)(2)(c) cha sheria hiyo.

Kwa msingi huo, alitaka Mahakama Kuu ibadilishe uamuzi wa Mahakama ya Wilaya na kumtia Mbukwa hatiani kwa kosa la usafirishaji haramu wa dawa za kulevya.

Mbukwa alipinga rufaa hiyo na kuomba Mahakama Kuu iendelee kuishikilia hukumu ya Mahakama ya Wilaya na kudai kuwa ushahidi uliothibitishwa mahakamani ulikuwa wa kumiliki bangi, siyo wa usafirishaji wa dawa za kulevya na kuomba rufaa ya DPP itupiliwe mbali.

Uamuzi Mahakama

Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu ilisema kiini cha kushindwa kwa DPP kilikuwa namna rufaa hiyo ilivyowasilishwa.

Mahakama ilibaini kuwa DPP alitoa taarifa ya nia ya kukata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya na  msingi wa rufaa uliowasilishwa ulikuwa mmoja kuwa hakimu alikosea kisheria kwa kutoa hukumu isiyofaa.

Kwa mujibu wa Mahakama, katika kesi za jinai kuna tofauti kati ya kupinga hatia na kupinga hukumu au adhabu.

Jaji Pomo amesema baada ya mshtakiwa kupatikana na hatia, mahakama hutoa adhabu na mhusika anaweza kukata rufaa dhidi ya hatia, adhabu au vyote viwili na kuwa jambo analolalamikia lazima lielezwe wazi katika taarifa ya nia ya kukata rufaa na katika misingi ya rufaa.

Mahakama ilisema DPP hakuwasilisha msingi wa rufaa uliopinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya wa kumtia Mbukwa hatiani chini ya kifungu cha 17 cha sheria tajwa juu.

Amesema badala yake, wakati wa kuwasilisha hoja za rufaa, DPP alitaka Mahakama Kuu itathmini upya ushahidi na kuamua kuwa Mbukwa alipaswa kutiwa hatiani kwa kosa tofauti la usafirishaji wa dawa za kulevya na hoja hiyo haikuendana na msingi wa rufaa uliowasilishwa.

Mahakama imesema kuwa upande unaokata rufaa hufungwa na misingi ya rufaa uliyoainisha na hauwezi kuibua hoja mpya wakati wa usikilizwaji wa rufaa kwa urahisi wake.

Jaji amesema iwapo DPP alitaka kupinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya wa kumtia Mbukwa hatiani chini ya kifungu cha 17, alipaswa kuweka wazi jambo hilo katika taarifa ya nia ya kukata rufaa na katika msingi wa rufaa.

Mahakama pia ilisema DPP hakupinga adhabu ya miaka mitatu kwa hoja kwamba ilikuwa kinyume na adhabu iliyowekwa kisheria kwa kosa ambalo Mbukwa alikutwa nalo, hivyo Mahakama kusema haikuona sababu ya kuingilia hukumu ya Mahakama ya Wilaya, ambayo ilitoa adhabu iliyokuwa ndani ya kiwango kilichowekwa na sheria.

Kwa kuzingatia hayo, Mahakama Kuu iliamua kuwa rufaa ya DPP haikuwa na msingi na kuiondoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *