Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty ameituhumu Ethiopia kuwa inasimamia Bwawa Kuu la Renaissance (GERD) kwenye Mto Nile “kwa njia ya kisiasa” kupitia hatua za upande mmoja dhidi ya Misri na Sudan.

Badr Abdelatty amesema hayo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Maria Manuela dos Santos Lucas mjini Cairo.

Abdelatty amesema kwamba suala la maji ni “la kufa na kupona” na ni kipaumbele cha juu kwa Misri, akisisitiza kwamba “haliwezi kufumbiwa macho.” Ameongeza kuwa Misri imeonya mara kwa mara kwamba Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance “lilijengwa kwa maamuzi ya upande mmoja, bila kuheshimu sheria za kimataifa na uratibu wa awali, na kwamba Ethiopia, kama nchi ya vyanzo vya Mto Nile, haiwezi kuchukua hatua za upande mmoja.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameeleza kwamba usimamizi wa bwawa hilo wa Ethiopia “kwa njia ya kisiasa” na bila uratibu wa awali na nchi za Misri na Sudan zinazopakana na mto huo una “athari mbaya sana,” akisisitiza kwamba kuzuia maji bila uratibu wa awali kumepelekea kupungua kwa viwango vya maji nchini Sudan katika siku za hivi karibuni, jambo ambalo limeathiri upatikanaji wake kwa Wasudani.

Abdelatty amesisitiza kwamba Misri “haipingani na haki ya Ethiopia ya kuwa na maendeleo, lakini bila kusababisha madhara kwa Sudan na Misri,” akiongeza kwamba “wana haki ya kupata maendeleo na sisi tuna haki ya kuishi.”

Ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile huko Ethiopia umeibua mvutano mkubwa wa maji kati ya nchi hizo tatu tangu mwaka 2011 hadi sasa.

Ethiopia kwa upande wake inalihesabu bwawa hilo lililogharimu karibu dola bilioni 5 kama ishara ya fahari ya kitaifa na muhimu kwa usambazaji wa nishati ya umeme na imekadhibisha vikali tuhuma za Misri kupitia taarifa mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *