Leo ni Jumatano tarehe 7 Safar 1448 Hijria sawa na Julai 22, 2026.

Katika siku kama ya leo miaka 1398 iliyopita, yaani tarehe 7 Safar mwaka 50 Hijiria kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).

Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake, Mtume Muhammad (saw) ambapo alinufaika na mafunzo na maarifa ya dini tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as).

Baada ya kuuliwa Imam Ali (as), Waislamu walimpa baia na mkono wa utiifu Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza; hata hivyo baada tu ya kushika hatamu alikabiliwa na njama na uasi wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi kwa ajili ya kukabilina na uasi wa Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah.

Imam Hassan al Mujtaba (as) alilazimika kufanya suluhu na Muawiyah bin Abi Sufiyan kwa ajili ya kulinda maslahi ya Uislamu na Waislamu. Mjukuu huyo kipenzi wa Mtume (saw) aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.   ****

Siku ya leo tarehe 7 Mfunguo Tano Safar inasadifiana na siku ya tukio la kuchimbwa handaki kandokando ya mji mtakatifu wa Madina kwa ajili ya kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya maadui wa Uislam. Siku hii ni siku ya kumkumbuka na kumuenzi Sahaba mwema wa Mtume Muhammad (SAW), Salman al Farisi (RA). 

 Salman Farisi alikuwa Muirani wa kwanza kuingia kwenye dini ya Uislamu. Alijipamba kwa sifa nyingi nzuri za uchamungu, maadili mema na tabia nzuri hadi akatambuliwa kuwa mmoja wa masahaba wa karibu wa Bwana Mtume SAW.

Salman al Farisi alishiriki kwenye vita mbalimbali dhidi ya maadui wa Uislamu. Alitoa mchango mkubwa katika ushindi wa jeshi la Kiislamu katika vita vya Khandak kwa pendekezo lake la kuchimbwa handaki kubwa kando kando ya mji wa Madina ili kuulinda mji huo.

Salman al Farisi aliaga dunia mwaka 34 Hijria katika mji wa Madain nchini Iraq na kuzikwa katika eneo hilo.    *****

Miaka 413 iliyopita katika siku kama ya leo, Mikhail Ramanov alikalia kiti cha utawala wa Russia na kwa utaratibu huo, utawala wa miaka 304 wa familia ya Ramanov ukawa umeanza nchini humo.

Miaka mitatu baada ya mashambulio ya vikosi vya Poland dhidi ya Russia, mmoja wa makamanda wa Kirusi alifanikwa kuvishinda vikosi hivyo na kuudhibiti mji wa Moscow. Baada ya jeshi la Poland kufukuzwa nchini humo, Mikhail Ramanov akashika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Katika kipindi cha utawala wa familia ya Ramanov, Russia ilipanuka lakini kwa upande wa uchumi haikupiga hatua kubwa.   ****

Katika siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, kulitokea vita maarufu vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Isonzo.

Vita hivyo vilitokea sambamba na kujiri Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Vita vya Isonzo vilitokea katika maeneo ya milimani yaliyojulikana kwa jina hilo hilo nchini Italia.

Vita hivyo vilikuwa baina ya jeshi la Italia lililokuwa katika safu ya waitifaki na Austria iliyokuwa upande wa Ujerumani. Watu wapatao 70,000 wengi wao wakiwa ni Wataliano waliuliwa katika vita vyab Isonzo. Pamoja na hayo, jeshi la Italia lilipata ushindi dhidi ya jeshi la Austria katika vita hivyo.  ***

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 1961, yalianza mapigano makali kati ya majeshi ya Ufaransa na Tunisia, baada ya vikosi vya Ufaransa kuushambulia mji wa kihistoria wa Bizerte ulioko kaskazini mashariki mwa Tunisia.

Mara baada ya Tunisia kujitawala kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1956, mkoloni huyo aliendelea kuikalia kwa mabavu bandari ya Bizerte, na kuifanya kuwa kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo.  

Hata hivyo majeshi ya Tunisia yalifanikiwa kuikomboa bandari hiyo kwenye mapigano hayo makali yaliyopelekea Watunisia 750 kuuawa.  ***

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, jeshi la mtawala wa wakati huo wa Iraq, dikteta Saddam Hussein lilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya maeneo ya kusini ya Iran.

Mashambulio hayo yalianza siku nne tu baada ya Iran kulikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lililokuwa limepasishwa takribani mwaka mmoja kabla, lilisisitiza juu ya usitishaji vita, liliuarifisha  utawala vamizi, likataka kulipwa fidia waathiriwa wa hujuma hiyo, kubadilishana mateka mataifa mawili ya Iran na Iraq na kurejea vikosi vya nchi mbili hizo katika mipaka ya kimataifa.

Utawala vamizi wa Iraq hapo kabla ulikuwa umelikubali azimio hilo na ulikuwa ukiendesha propaganda dhidi ya Iran kutokana na kutolikubali azimio hilo. Lakini wakati Iran pia ilipotangaza kulikubali azimio hilo, jeshi la dikteta Saddam kwa mara nyingine tena likaishambulia ardhi ya Iran. ***

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, ndege za kivita za utawala wa Israel zilishambulia eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina, na kuua watu 16 na wengine 150 kujeruhiwa.

Shambulio hilo la kushtukiza lililofanyika usiku, liliua watoto 9 wasiokuwa na hatia yoyote. Hali kadhalika miongoni mwa waliouawa shahidi katika shambulizi hilo ni Sheikh Swalah Shahadah, mmoja wa makamanda wa Brigedi ya Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya kiislamu ya Palestina HAMAS ambaye aliuawa akiwa pamoja na mkewe na binti yake.    ****

Miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 22 Julai 2003, waliuawa Uday na Qusay watoto wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq pambizoni mwa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq.

Uday na Qusay wakiwa wamefuatana na maafisa wa ngazi za juu wa Iraq walitoroka mjini Baghdad baada ya majeshi ya Marekani na Uingereza kuishambulia nchi hiyo mwezi Aprili 2003.

Majeshi ya Marekani yalishambulia nyumba walimokuwa wamejificha watoto hao wa Saddam Hussein na kuwauwa pamoja na wasaidizi wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *