Rais Donald Trump alitoa wito wa kusitishwa mashambulizi kwa Israel , mshirika mkuu wa Marekani, baada ya kundi la wanamgambo wa Kipalestina, Hamas, kusema kuwa liko tayari kuwaachilia mateka wote na kuanza mazungumzo kuhusu mpango wake wa kumaliza vita vilivyodumu kwa takriban miaka miwili.
Katika taarifa iliotolewa Ijumaa kundi la Hamas lilitangaza kuidhinisha kuachiliwa kwa mateka wote — walio hai na waliopoteza maisha — kwa mujibu wa mpango wa kubadilishana uliomo katika pendekezo la Rais Trump.
Baadaye Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba “Kwa kuzingatia taarifa iliyotolewa na Hamas, naamini wako tayari kwa AMANI ya kudumu. Israel lazima isitishe mara moja mashambulizi ya Gaza ili tuweze kuwaokoa mateka kwa usalama na haraka!”
Afisa mwandamizi wa Hamas alisema Jumamosi kuwa kundi hilo “liko tayari kuanza mazungumzo mara moja ili kukamilisha masuala yote.”
Afisa mwingine wa Hamas alisema kuwa Misri, mpatanishi katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, itakuwa mwenyeji wa mkutano wa makundi ya Kipalestina ili kuamua mustakabali wa Gaza baada ya vita.
Pendekezo la Trump linataka kusitishwa kwa mapigano, kuachiliwa kwa mateka ndani ya saa 72, kuondoka kwa majeshi ya Israel hatua kwa hatua kutoka Gaza, na kuharibiwa kwa silaha za Hamas.
Pia linabainisha kuwa Hamas na makundi mengine “hayatakuwa na nafasi yoyote katika uongozi wa Gaza”, ambapo usimamizi wa eneo hilo utachukuliwa na chombo cha kiteknokrasia kitakachosimamiwa na mamlaka ya mpito baada ya vita, chini ya Trump mwenyewe.
“Hitaji la Rais Trump la kusitisha vita mara moja ni muhimu ili kuzuia madhara makubwa na yasiyorekebishika kwa mateka,” limesema Jukwaa la Familia za Mateka na Waliopotea katika taarifa.
“Tunamwomba Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aanze mara moja mazungumzo ya haraka na yenye ufanisi ili kuwarudisha mateka wetu wote nyumbani.”
Mashambulizi Makali ya jeshi la Israel
Lakini licha ya wito wa Trump, kitengo cha ulinzi wa raia wa Gaza kilisema kuwa Israel ilitekeleza mashambulizi kadhaa katika Jiji la Gaza usiku kucha, huku hospitali za karibu zikiripoti majeruhi.
“Usiku ulikuwa wa vurugu sana, ambapo jeshi la Israel lilifanya mashambulizi ya anga na mizinga katika Jiji la Gaza na maeneo mengine ya Ukanda huo, licha ya wito wa Rais Trump wa kusitisha mashambulizi,” msemaji wa kitengo cha ulinzi wa raia wa Gaza Mahmud Bassal aliiambia AFP.
Bassal, ambaye kitengo chake ni kikosi cha uokoaji kinachofanya kazi chini ya mamlaka ya Hamas, alisema nyumba 20 zilibomolewa usiku huo.
Jeshi la Israel lilisema linaendelea na operesheni zake katika Jiji la Gaza na likawaonya wakazi wasirudi.
“Wanajeshi wa IDF bado wanafanya operesheni katika Jiji la Gaza, na kurudi huko ni hatari sana. Kwa usalama wenu, epukeni kurudi kaskazini au kukaribia maeneo ya shughuli za wanajeshi wa IDF — hata katika Ukanda wa Gaza wa kusini,” alisema msemaji wa jeshi kwa lugha ya Kiarabu, Kanali Avichay Adraee, kupitia X.
Nafasi ya kumaliza “umwagaji damu” huko Gaza
Mkuu wa Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amesema Jumamosi kuwa mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Gaza ni “fursa muhimu” ya kusitisha umwagaji damu na mateso katika eneo la Palestina “moja kwa moja.”
“Hii ni fursa muhimu kwa pande zote na mataifa yenye ushawishi kuifuatilia kwa nia njema na kusitisha — moja kwa moja — mauaji na mateso huko Gaza, kulijaza eneo hilo kwa msaada wa kibinadamu, na kuhakikisha kuachiliwa kwa mateka pamoja na Wapalestina wengi waliokamatwa,” ofisi yake ilisema kupitia X.
Wakati huo huo, ,maafisa wa Uturuki wamesema kuwa raia 36 wa Kituruki na raia kutoka nchi 12 walitarajiwa kuwasili Istanbul siku ya Jumamosi kwa ndege maalum, baada ya Israel kuzuia msafara wa misaada uliokuwa ukielekea Gaza na kuwakamata mamia ya watu.
Chanzo cha kidiplomasia kutoka Uturuki kilisema kuwa ndege hiyo ilikuwa imebeba watu 137 waliokuwemo katika msafara huo, wakiwemo raia 36 wa Uturuki.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Oncu Keceli, alitangaza mapema Jumamosi kuwa ndege maalum ilikuwa imekodishwa kuwarejesha wanaharakati waliokamatwa kutoka Israel.
Uturuki imetaja hatua ya Israel ya kuzuia msafara huo kuwa “kitendo cha kigaidi”, na Alhamisi ikasema imeanzisha uchunguzi baada ya vikosi vya Israel kuwakamata raia wa Uturuki waliokuwa ndani ya msafara huo.