
Ukiwa umepita mwaka mmoja na miezi sita katika uongozi wa juu, John Heche ameendelea kuongoza mapambano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika kupigania Katiba mpya kwa mustakabali mwema wa taifa hili.
Tangu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu alipokamatwa, Aprili 9, 2025, Heche ameshika usukani katika chama hicho akiongoza mapambano hayo huku ikiongezwa ajenda nyingine ya kutaka Lissu aachiwe huru.
Safari ya uongozi ya Heche, ilianza rasmi Januari 22, 2025 baada ya kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Chadema katika uchaguzi uliojaa ushindani mkali ulioambatana na matusi, kashfa na kutuhumiana.
Heche, akiwa kwenye kambi ya Lissu, walifanikiwa kushinda uchaguzi huo dhidi ya kambi ya Freeman Mbowe, aliyekuwa akitetea nafasi yake ya mwenyekiti, pamoja na Ezekia Wenje aliyekuwa akigombea nafasi ya makamu mwenyekiti Tanzania Bara.
Baada ya uchaguzi huo uliotikisa na kutoa somo kwa vyama vingine, kambi ya Lissu iliyoshinda ilianza kazi mara moja huku ikibeba ajenda ya “No reforms, No election” (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi), ikishinikiza kutofanyika kwa uchaguzi hadi mabadiliko yatakapofanyika.
Sasa ni mwaka mmoja na miezi sita, Heche akiwa ndiye kiongozi wa Chadema, amekutana na mambo mengi yanayoweza kumfanya akate tamaa na kurudi nyuma, lakini amekuwa kiongozi imara akiwa tayari kusonga mbele.
Makala haya yanaangazia mitihani mikuu aliyopitia kiongozi huyo tangu amekuwa kiongozi huku mwenyewe akieleza namna anavyozikabili changamoto hizo kwa ujasiri na dhamira iliyo ndani yake.
Uongozi wa chama
Baada ya kukamatwa kwa Lissu, Aprili 9, 2025, Heche amekuwa kiongozi wa Chadema, chama kilichopitia misukosuko mingi tangu uchaguzi wa ndani wa Januari 21, 2025 ikiwamo kuondokewa na wanachama waandamizi.
Heche anaongoza chama ambacho hadi sasa hakina ruzuku iliyozuiliwa baada ya mmoja wa waliokuwa viongozi wake kufungua shauri mahakamani akidai kwamba hakuna mgawanyo sawa wa rasilimali ndani ya chama hicho kati ya bara na Zanzibar.
Mzigo wa kukiendesha chama hicho kilichogawanyika, chenye upungufu wa rasilimali na kinachobeba matumaini ya wananchi, uko mikononi mwa Heche kwa sasa huku naye akipita kwenye nyakati ngumu ambazo zinaweza kumtikisa mtu dhaifu.
Hata hivyo, ameendelea kuongoza operesheni za Chadema kwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini huku mapokezi yao yakiwa makubwa kila wanakopita, jambo linaloashiria matumaini ya watu kwa chama hicho.
Akamatwa Dar es Salaam
Oktoba 22, 2025, Heche alikamatwa na Jeshi la Polisi kwenye geti la Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam alikokwenda kusikiliza kesi ya Lissu, kwa madai kwamba alivuka mpaka kuingia nchi jirani ya Kenya kinyume cha sheria.
Novemba 10, 2025, Heche pamoja na viongozi wengine wa Chadema waliokuwa wamekamatwa, waliachiwa huru, akiwa amekaa mahabusu kwa takribani wiki tatu tangu alipokamatwa.
Kukamatwa kwa Heche kuliibua sintofahamu baada ya familia kujitokeza na kudai kwamba hawajui mahali ndugu yao anaposhikiliwa licha ya kuzunguka katika vituo mbalimbali vya polisi kuulizia alipo ndugu yao.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilijitokeza na kueleza linamshikilia kiongozi huyo kabla ya kumwachia huru kwa dhamana. Aliendelea na shughuli zake za kisiasa kama kiongozi wa Chadema, akikutana na wananchi.
Dereva wake afariki
Wakati akiwa kwenye ziara zake za kikazi, Julai Mosi, 2026, dereva wa Heche, Suez Maradafu alifariki dunia katika nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia mkoani Kigoma.
Taarifa za kifo cha Maradafu zilitolewa awali na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Goluwa, aliyesema mwili wa marehemu ulikutwa ndani ya nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia, ukiwa karibu na mlango wa chumba chake.
Mazingira ya kifo cha dereva huyo yalijaa utata, jambo lililosukuma haja ya kufanyika kwa uchunguzi maalumu ili kubaini chanzo cha kifo chake na kama kuna uhusika wa mtu yoyote katika kifo hicho.
Uchunguzi ulifanywa na jopo la madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, wataalamu kutoka Wizara ya Afya Dodoma pamoja na ofisa kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Kifo cha Maradufu kimekuwa pigo kubwa kwa Heche kama alivyoeleza mwenyewe kwenye mazishi yake, akisema alifahamiana naye tangu alipokuwa mdogo na alikuwa sehemu ya familia yake kwa kipindi kirefu.
Tuhuma za ubadhirifu
Wakati akiomboleza kifo cha dereva wake, baadhi ya makada na viongozi wa Chadema wamejitokeza hadharani wakimtuhumu Heche kula fedha za michango, wakitaka achukuliwe hatua za kinidhamu.
Makada hao ambao wengine ni viongozi wa chama hicho, wameshusha lawama dhidi ya Heche wakidai kwamba ametumia michango inayotolewa na wadau wa wananchi kwa maslahi yake binafsi.
Hata hivyo, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Mkoa wa Mara waliofika nyumbani kwake wilayani Tarime, Heche alisema hatishiki na mashambulizi yanayoelekezwa dhidi yake, akijifananisha na mchezaji hatari uwanjani anayekabwa zaidi.
Licha ya kuwapo kwa tuhuma hizo, kwenye mitandao ya kijamii, wananchi wanaoandika wanakataa tuhuma hizo huku wakidai kwamba ni mpango wa kufifisha harakati za Heche na chama chake katika kupigania demokrasia ya kweli nchini.
Mwenyewe hana hofu
Akizungumza na Mwananchi kuhusu sekeseke analopitia, Heche anasema mitihani kwa mwanasiasa wa upinzani hasa kwenye nchi zenye baadhi ya watu wasiostaarabika, ni mambo ya kawaida.
“Watu wamepitia mitihani mikubwa, kuna watu wamekufa, watu wamepotea, mimi mwenyewe nimepoteza mdogo wangu tumbo moja damu moja. Mimi naamini hii ni mitihani ya kawaida na nasonga mbele,” anasema.
Kwa mwanasiasa wa namna yake, anasema kurushiwa uchafu ni jambo la kawaida, akitolea mfano historia ya Nabii Yusuph aliyezushiwa kesi ya ubakaji na kufungwa jela miaka 13 na baadaye akawa Waziri Mkuu wa Misri.
“Haya mambo yapo, lakini mimi nimejikita kujadili masuala ya wananchi. Mambo ya Katiba mpya, mwenyekiti wetu, Tundu Lissu atatokaje ili aje tuendeleze mapambano,” anasema Heche.
Msisitizo wa Heche kuhusu mitihani hiyo, anasema yaliyomtokea na yatakayomtokea atayakabili kwa kuwa ana nguvu za kutosha na hakuna mtu atakayemudu kumtoa kwenye reli.
Pia, anasema ana uzoefu wa kutosha kwenye siasa kwani amepita njia zote za uongozi kuanzia chini hadi alipo sasa, hivyo anamudu kuyakabili yote yanayolengwa kwake.
“Bahari iliyotulia haileti nahodha bora. Huwezi kupima nahodha bora wa chombo kwa bahari iliyotulia. Tangu mwenyekiti wetu amekamatwa utaona chama kimeendelea na shughuli zake, tumefanya mikutano hapa ilikuwa balaa, hiyo inatosha kuonyesha kuwa nahodha aliyepo sio wa kutiliwa shaka,” anasisitiza Heche.
Mtihani wa uongozi
Akizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa, Dk Amani Mwakifule anasema mfululizo wa matukio yanayomkumba Heche tangu kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara unaweza kutazamwa kama mtihani wa uongozi unaopima uwezo wake wa kustahimili shinikizo la kisiasa na binafsi.
Anasema kufiwa na dereva wake wa muda mrefu, kukamatwa na kushikiliwa na vyombo vya dola pamoja na kufanya kazi wakati mwenyekiti wake akiwa gerezani, kumemweka kwenye mazingira yanayohitaji uimara wa kiakili na kisiasa.
Dk Mwakifule anasema tuhuma za matumizi mabaya ya michango, hata kabla ya kuthibitishwa, zinaweza kuathiri taswira ya kiongozi kwa sababu zinagusa suala nyeti la uaminifu wa wanachama na wafadhili wa chama.
Hata hivyo, anasema historia ya siasa za upinzani inaonyesha kuwa viongozi wanaopitia misukosuko mikubwa mara nyingine hujijengea mtaji wa kisiasa iwapo wanachama wataamini wanakabiliwa na mashinikizo kutokana na misimamo yao.
“Matokeo yake itategemea namna atakavyosimamia tuhuma zinazomkabili na kuendelea kuunganisha chama. Akivuka kipindi hiki bila kupoteza uungwaji mkono, anaweza kutoka akiwa na ushawishi mkubwa zaidi ndani ya Chadema,” anasema Dk Mwakifule.
Uenyekiti umemponza
Mchambuzi wa siasa, Profesa Baraka Mfinanga anasema mlolongo wa matukio yanayomkumba Heche unapaswa kutazamwa katika muktadha wa nafasi yake mpya ya uongozi ndani ya Chadema na mazingira ya kisiasa yanayokikabili chama hicho.
Anasema viongozi wanaopanda ngazi za juu za vyama vya siasa mara nyingi huingia katika kipindi ambacho kila hatua yao huangaliwa kwa karibu na marafiki pamoja na wapinzani wao wa kisiasa.
“Kufiwa na dereva wa muda mrefu ni pigo lenye athari za kibinadamu na kisiasa kwa sababu limetokea wakati Heche akiwa katikati ya majukumu makubwa ya chama,” anasema.
Anaeleza kuwa matukio ya kukamatwa, kushikiliwa au kukabiliwa na mashauri huongeza taswira ya kiongozi anayepitia mazingira magumu, jambo linaloweza kuzalisha huruma au mshikamano kutoka kwa wafuasi wake.
Profesa Mfinanga anasema kuwapo kwa mwenyekiti wa chama gerezani kumemlazimu Heche kubeba sehemu ya mzigo wa kisiasa, hali inayoongeza matarajio ya wanachama kuhusu uwezo wake wa kuongoza.
Kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya michango, anasema hizo ni tuhuma zinazogusa moja kwa moja suala la uadilifu, ambalo ni mtaji muhimu kwa mwanasiasa anayetarajia kuaminika mbele ya wanachama.
“Hata kama tuhuma hazijathibitishwa, athari yake kubwa huwa kwenye taswira. Katika siasa, mara nyingi mtazamo huwa na uzito sawa na ukweli mpaka pale ufafanuzi kamili unapopatikana,” anasema.
Kwa maoni yake, iwapo Heche ataweza kuvuka kipindi hiki huku akiendelea kuungwa mkono na wanachama, matukio hayo yanaweza kumjengea hadhi ya kiongozi aliyepitia majaribu makubwa na kubaki imara kisiasa.