
Dar es Salaam. Simba haikukurupuka kumtambulisha Selemani Mwalimu.
Kilichotokea ni kwamba mabingwa hao wa Kombe la FA waliamini kila kitu kilikuwa kimekamilika baada ya kutuma fedha za mkataba wa mkopo, lakini baadaye ikabainika kuwa malipo hayo yaliingia kwenye akaunti ya zamani ya Wydad AC, jambo lililosababisha miamba hiyo ya Morocco kutangaza kuwa mshambuliaji huyo bado ni sehemu ya kikosi chao.
Taarifa ambazo Mwananchi imezipata kutoka kwa mtu wa karibu na mchezaji huyo zinaeleza kuwa Simba na Wydad tayari walikuwa wamefikia makubaliano ya Mwalimu kuendelea kuitumikia Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja, huku upande wa Simba ukitekeleza masharti ya awali kwa kutuma fedha zilizokubaliwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baada ya kukamilisha hatua hiyo Simba iliamini dili hilo limekamilika na ndipo ikamtangaza hadharani Mwalimu kama sehemu ya kikosi chake kitakachoshiriki msimu mpya wa mashindano.
Hata hivyo wakati Simba ikitangaza usajili huo, viongozi wa Wydad walipofanya uhakiki wa miamala kwenye akaunti yao rasmi hawakuona fedha zozote zikiwa zimeingia. Hata hivyo uchunguzi ulibaini kuwa malipo hayo yalikuwa yamepelekwa kwenye akaunti ya zamani ya klabu hiyo ambayo tayari ilikuwa imebadilishwa.
“Makubaliano yalishafanyika na Simba walikuwa wametekeleza upande wao. Tatizo lilikuwa fedha kuingia kwenye akaunti ya zamani ya Wydad walipoangalia akaunti wanayotumia sasa hawakuona malipo yoyote, ndipo wakaamini dili halijakamilika na kutoa taarifa kwamba mchezaji bado ni sehemu ya kikosi chao,” kimesema chanzo hicho.
Taarifa ya Wydad imeonekana kuzua taharuki kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya mashabiki wakijiuliza ni ipi taarifa sahihi kati ya ile ya Simba iliyomtambulisha Mwalimu na ile ya mabingwa hao wa Morocco waliodai bado wanamhitaji mshambuliaji huyo.
Taarifa zinaeleza kuwa pande zote mbili zinafanyia kazi kurekebisha hitilafu hiyo ya kifedha kwa kuzirejesha fedha kutoka kwenye akaunti ya zamani ili ziingizwe kwenye akaunti rasmi ya Wydad.
Mchakato huo ukikamilika, klabu hiyo ya Morocco inatarajiwa kuthibitisha rasmi makubaliano ya kumruhusu Mwalimu kuendelea kuitumikia Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Chanzo hicho kinasisitiza kuwa hakuna mgogoro wowote kati ya Simba na Wydad kuhusu mchezaji huyo, bali kilichotokea ni hitilafu ya kiutawala katika miamala ya fedha.
Simba iliamua kupambana kumbakiza Mwalimu baada ya kuridhishwa na kiwango alichoonyesha msimu uliopita. Mshambuliaji huyo alikuwa mmoja wa nyota muhimu wa kikosi hicho baada ya kufunga mabao 15 katika mashindano yote, akitoa mchango mkubwa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.