Rais wa heshima wa Simba SC, Mohammed Dewji ‘MO’ ameongoza mamia ya waombolezaji kwenye mazishi ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo, Idd Kajuna.

MO amefika kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori katika mazishi hayo yaliyofanyika jioni ya leo Julai 23, 2026.

Mbali na MO, Makamu wa Rais wa Yanga SC, Arafat Haji naye ameshiriki mazishi hayo sambamba na wadau mbalimbali wa klabu hiyo huku pia Makamu wa Rais wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ naye akiwa sehemu wa waombolezaji.

Akizungumza baada ya mazishi hayo, Arafat amesema Yanga imepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Kajuna na kwamba Simba wamepata pigo kwa kumpoteza kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kuipigania klabu hiyo.

“Nipo hapa kuiwakilisha klabu ya Yanga, huu ni msiba mkubwa kwenye michezo hususan soka, tukio kama hili linatuunganisha kama familia ya soka, upinzani wa klabu zetu tunaweka pembeni,” amesema Arafat.

“Wakati tunapokea taarifa hii Rais wangu (Hersi Said) alikuwa anaanza safari, nikamwambia wewe nenda mimi nitakuja kushiriki msiba huu na watani wetu, Simba imepata pigo kubwa kwa kumpoteza Kajuna.”

Naye Popat amesema Kajuna alikuwa kiongozi mzuri, ambaye mara ya mwisho alikutana naye Pemba, kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambapo amewapa pole Simba kwa msiba huo.

“Tuko hapa kumsindikiza mwenzetu ambaye leo ametangulia na sisi tutafuata, tumempoteza mwenzetu kwenye tasnia ya michezo hasa soka, licha ya kwamba yeye (Kajuna) alikuwa Simba lakini sisi ni familia moja, hivi karibuni binafsi nilikutana naye Pemba kwenye fainali, tuliongea, sasa unapopata taarifa kama hii lazima inashtua na kuumiza, tunawapa pole wenzetu wa Simba kwa msiba huu,” amesema Popat.

Kajuna amefariki usiku wa kuamkia leo Julai 23, 2026 katika Hispitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha Moyo baada ya kupumzishwa hapo kwa siku saba.

Mpaka anafariki, Kajuna alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Simba, ambapo pia amewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *