TAARIFA kutoka ndani ya Yanga zinabainisha kuwa, beki wa kulia wa timu hiyo, Kibwana Shomari, ameongezewa mkataba mpya, hivyo ataendelea kuwa sehemu ya kikosi hicho kwa miaka miwili hadi 2028.

Mwanaspoti limepata taarifa hizo kutoka kwa mtu wa karibu na Kibwana aliyesema tayari beki huyo ameshasaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia klabu hiyo.

“Mkataba wake uliisha, viongozi walifanya naye mazungumzo mapya, wamefikia makubaliano na uamuzi wa mwisho amesaini miaka miwili ili kuendelea kuitumikia Yanga ambayo imebadilisha maisha yake kutoka hatua moja kwenda nyingine kiuchumi tangu alipojiunga nayo akitokea Mtibwa,” kilisema chanzo hicho.

Beki huyo alijiunga na Yanga Agosti 9, 2020 akitokea Mtibwa Sugar, tangu hapo, amekuwa na vipindi vya kupanda na kushuka kutokana na nafasi yake kikosini akiwa sehemu ya mafanikio ya kubeba mataji matano mfululizo ya Ligi Kuu kuanzia 2021-2022 hadi 2025-2026. Pia mataji manne ya Kombe la FA.

Kitendo cha Kibwana kusalia kwake Yanga, kumeibua mastaa wa zamani walioona ni beki mzuri, endapo akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara, atakuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo.

Beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua, amesema: “Kibwana ni beki mzuri, hadi viongozi wameamua kumuongeza mkataba wameona huduma yake inahitajika.”

Beki mwingine wa zamani wa timu hiyo, Ladislaus Mbogo, amesema: “Mchezaji anapopata nafasi kwanza anakuwa anajiamini na kiwango chake kinakuwa bora, naamini akipata nafasi ya kucheza chini ya kocha mpya basi atakuwa na mchango mkubwa kikosini.”

Wengine ambao wameongeza mikataba ndani ya Yanga kuelekea msimu ujao baada ya kumalizika, ni kipa Hussein Masalanga na Kouassi Attohoula Yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *