
NAHODHA wa Timu ya Taifa ya Soka Wanawake Tanzania, Twiga Stars, Opah Clement, amesema mechi za kirafiki ambazo timu hiyo imecheza zimekuwa na mchango mkubwa kwenye maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026.
Opah ameeleza kuwa, mechi walizocheza dhidi ya Ghana na Nigeria zimewapa picha halisi ya kiwango walichonacho na maeneo yanayohitaji kuboreshwa kabla ya kuanza kwa mashindano.
Mshambuliaji huyo amesema mechi hizo zimempa kocha nafasi ya kutathmini kikosi na kwamba kila mchezaji yuko tayari na anaelewa wajibu wake kuelekea mashindano yatakayoanza Julai 26, 2026 nchini Morocco.
“Tumepata ladha ya mechi inakuwaje kwenye mashindano kwa sababu tuliocheza nao wanashiriki WAFCON na kocha ameona kupitia mechi hizi za kirafiki. Sisi kama wachezaji mashindano yametupa mwanga wa tuko wapi na nini tunapaswa kufanya,” amesema nahodha huyo.
Licha ya kutopata matokeo waliyoyatarajia katika mechi hizo, Opah amesema timu imeimarika hasa kwenye eneo la mipira iliyokufa ambayo iliwagharimu katika mechi dhidi ya Ghana waliyopoteza kwa mabao 4-0.
“Hatujapata matokeo mazuri lakini ni moja ya mafanikio makubwa. Tumerekebisha vitu vingi, mechi ya kwanza dhidi ya Ghana tulifungwa mabao manne, kati ya hayo matatu yalitokana na set pieces (mipira ya kutengwa), tumeboresha sana eneo hilo na tumelifanyia kazi,” ameongeza.
Katika WAFCON 2026, Twiga Stars imepangwa Kundi B pamoja na mabingwa watetezi Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso.
Mashindano ya WAFCON 2026 yatafanyika nchini Morocco kuanzia Julai 26 hadi Agosti 16, 2026. Twiga Stars, hii itakuwa mara ya tatu kushiriki baada ya mwaka 2010 na 2024, ambapo iliishia hatua ya makundi.