Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kwamba mashambulizi makubwa ya anga ya utawala wa Israel eneo la Ukanda wa Gaza katika saa kadhaa zilizopita ni mwendelezo wa vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wasio na hatia na msisitizo wa kuvuruga makubaliano ya kusitisha mapigano.

Taarifa ya harakati ya Hamas imesisitiza kwamba baraza la mawaziri la utawala wa kigaidi wa Israel linataka kuzidisha mashambulizi, kukwepa majukumu yake yote chini ya makubaliano ya Sharm el-Sheikh na kuendeleza vita vya kikatili na mauaji na uharibifu katika Ukanda wa Gaza; vita ambavyo havijasimama hata kwa siku moja tangu kusainiwe makubaliano hayo.

Hamas imeitaka serikali ya Marekani, kama mwangalizi wa makubaliano ya kusitisha vita ya Sharm el-Sheikh, nchi wadhamini na wapatanishi, kutenda kama wapatanishi ili kukabiliana na uhalifu wa utawala ghasibu wa Israel na baraza la mawaziri la mhalifu wa kivita Benjamin Netanyahu, na kuulazimisha utawala huo kuacha ukiukaji wa sheria na uchokozi wake dhidi ya watu wa Palestina wasio na ulinzi.

Vyanzo vya habari viliripoti usiku wa kuamkia leo kwamba jeshi la Israel limeshambulia majengo matatu ya makazi ya raia katika Ukanda wa Gaza katika uhalifu wake wa hivi karibuni zaidi dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo.

Ripoti zinasema ndege za kivita za Israel zimelenga jengo la makazi ya raia katika kitongoji cha Al-Zaytoun kusini mashariki mwa Jiji la Gaza kwa makombora mawili.

Ndege za kivita za Israel pia zimelipua majengo mengine mawili ya raia katika kambi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na katika kambi ya Al-Bureij katikati mwa ukanda huo.

Hakuna ripoti zilizotolewa bado kuhusu walengwa wa mashambulizi hayo matatu wala idadi ya waliouawa na kujeruhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *