Leo ni Ijumaa tarehe 9 Safar 1448 Hijria sawa na tarehe 24 Julai mwaka 2026.

Siku kama ya leo miaka 243 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela.

Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia

Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea pia hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru.   ****

Miaka 224 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas.

Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa.   ****

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa.

Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa ulihalalisha suala hilo.    ****

Katika siku kama ya leo miaka 99 iliyopita yaani tarehe 24 Julai 1927, aliaga dunia mwandishi mkubwa na mwanafasihi wa Japan, Ryunosuke Akutagawa.

Baada ya kumaliza masomo yake, aliandika hadithi maarufu “Rashōmon”. Katika maandishi yake, analaani vikali kujiona na ubinafsi uliokita mizizi kenye asili ya mwanadamu, jambo ambalo ndilo dhamira kuu ya kazi zote za Akutagawa.

Mwandishi huyo anahesabika kuwa mmoja wa waasisi wa kanuni mpya za fasihi huko Japan. Akutagawa ameacha athari muhimu ikiwa ni pamoja na vitabu vya “Binti wa Buibui” na “Tushi Gun.”   ***

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita kikosi cha anga cha jeshi la Uingereza kiliishambulia vikali bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Mashambulizi ya anga ya Ujerumani na Uingereza yalianza mwanzoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na kushadidi zaidi baadaye. Kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi mbili hizo waliuawa katika mashambulizi hayo.

Makumi ya maelfu ya raia wa kawaida waliuawa kwa umati katika mashambulizi ya kikosi cha anga cha Uingereza dhidi ya bandari ya Hamburg mbali na kuangamizwa taasisi kadhaa za kijeshi na kiuchumi. ***

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, baada ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini na vyombo vya usalama vya utawala wa Shah, maulamaa kadhaa na marajii kutoka Qum na Mash’had na miji mingine ya Iran walifunga safari na kuelekea Tehran.

Mbali na kuandika barua wakithibitisha daraja ya Umarjaa ya Imam Khomeini walitoa wito wa kuachiliwa huru mwanazuoni huyo. Hatua hiyo sambamba na kuendelea upinzani wa wananchi dhidi ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini, kuliulazimisha utawala wa Shah kumhamisha kiongozi huyo kutoka jela na kumpeleka katika nyumba moja ili kuwatuliza maulama na wananchi hao.

Siasa hizo za kutuliza mambo hazikuwa na taathira na kwa msingi huo utawala wa Shah, ukiwa na lengo la kuweka pengo baina ya Imam Khomeini na wafuasi wake, uliamua kumpeleka uhamishoni mwanazuoni huo nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye nchini Iraq. ****

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *