Dar es Salaam. Rais mstaafu, hayati Benjamin Mkapa ameeleza katika kitabu chake namna uhusiano wa Tanzania Bara na Zanzibar ulivyokuwa mgumu wakati wa uongozi wake na jitihada alizozifanya ili Muungano wa pande hizo mbili uendelee kuimarika.

Leo, Julai 24, 2026, hayati Mkapa ametimiza miaka sita tangu alipofariki dunia, Julai 24, 2020, akiacha alama zinazokumbukwa na Watanzania kupitia kaulimbiu yake ya “Ukweli na Uwazi” katika kipindi cha utandawazi.

Wakati Mkapa alipogombea urais uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, alijulikana kwa jina la ‘Mr Clean’ likimaanisha kuwa, alikuwa mgombea aliyekuwa akionekana kutokuwa na makandokando au tuhuma za ufisadi katika historia yake ya kisiasa.

Katika kitabu chake cha My Life, My Purpose: A Tanzanian President Remembers, Mkapa ametenga sura nzima kuelezea changamoto na ugumu aliokumbana nao wakati wa uongozi wake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.

Anaeleza jinsi alivyokabiliana na uamuzi magumu wa kisera, shinikizo la kisiasa, pamoja na juhudi za kusimamia mageuzi ya kiuchumi na kuimarisha utawala bora.

Mkapa anaeleza kwamba, uhusiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano yalikuwa nyeti kwa kiasi fulani katika kipindi chake cha uongozi, aliweza kutatua tofauti zilizojitokeza, kwa kuwa aliamini Muungano kama tunavyouita.

Anasema Muungano ni muhimu kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa sababu uchumi wa pande zote mbili umefungamana kutokana na ukaribu wetu wa kijiografia. Aidha, unasaidia kulinda usalama wa maeneo yote mawili.

Zaidi ya hayo, anasema gharama za kuendesha dola ya kisasa iliyo huru kikamilifu zingekuwa kubwa mno kwa eneo dogo kama Zanzibar na zingeweza kuirudisha nyuma kiuchumi.

Hata hivyo, wakati mwingine alijiuliza iwapo angeweza kuchukua hatua zaidi za kuimarisha Muungano, kwa kuwa baadhi ya Wazanzibari bado wanaamini kwamba, Tanzania Bara wanawakandamiza na masuala ya mamlaka kamili ya Zanzibar yameendelea kujitokeza mara kwa mara kama chanzo cha mvutano.

Kwa masikitiko, mahusiano hayo yamekuwa ya tahadhari na yenye misuguano kwa miongo kadhaa.

Anakumbuka Hassan Nassor Moyo na Salim Said Rashid, waliokuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri la kwanza la Baraza la Mapinduzi, walimwambia kwamba, kuelekea mwisho wa maisha ya Sheikh Abeid Amani Karume, uhusiano kati yake na Mwalimu Nyerere ulikuwa umeingia dosari.

“Kimsingi, tatizo la Zanzibar limekuwa uhasama uliokithiri kati ya chama tawala na chama cha upinzani. Bila kujali kama uhasama huo unatokana na historia au mitazamo potofu, ulikuwa na bado unaendelea kuwa jambo linalonisumbua na kunipa wasiwasi,” ameandika hayati Mkapa.

Salmin na muhula wa tatu

Hayati Mkapa anasimulia katika kitabu chake kwamba alikuwa na msongo mkubwa wa mawazo wakati Rais wa Zanzibar wakati huo, Dk Salmin Amour, alipotaka kuongeza muda wake wa uongozi na kugombea muhula wa tatu ambao haukuwa Kikatiba.

Anasema kilikuwa kipindi kigumu kwake kwa sababu hakutaka kuonekana kama anawaamulia au kuwaelekeza Wazanzibari nini cha kufanya, lakini wakati huohuo alikuwa na wajibu wa kulinda kanuni ya ukomo wa mihula miwili ya urais.

Pia, alikuwa akitambua historia ya wakati Mwalimu Nyerere alipomuondoa madarakani Rais wa pili wa Zanzibar, marehemu Aboud Jumbe.

“Ingawa nilikuwa nimepokea wajumbe kadhaa wa wazee kutoka Zanzibar waliokuwa wakishinikiza Rais Amour apewe nafasi ya kugombea muhula wa tatu, ndani ya moyo wangu nilijua kwamba Zanzibar ilikuwa na watu wengi wenye uwezo ambao wangeweza kupatikana na kuwa wagombea wapya wa urais.

“Hakukuwa na sababu ya kipekee iliyomfanya Amour aongeze muda wake wa uongozi. Kwa kweli, hoja yake ya kutaka muhula wa tatu haikuwa na msingi wa kutosha,” anaeleza Mkapa katika kitabu chake.

Anasema kama Rais wa Muungano na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), jukumu la kuwa mkali liliangukia kwake.

Kwa mujibu wa Mkapa, alidhamiria kutoruhusu Katiba ibadilishwe ili kumpa nafasi ya muhula wa tatu.

Hivyo, anaeleza kuwa alifanya maandalizi muhimu kwa kile alichohofia kingekuwa kikao chake kigumu cha kukabiliana na Amour katika mkutano wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM mapema Machi 2000.

“Uamuzi wa mwisho ulifanywa na Kamati Kuu ya Taifa; haukuwa uamuzi wangu binafsi, ingawa nilikuwa mwenyekiti wa kikao hicho. Nilieleza hoja zilizokuwa pande zote mbili, nikaruhusu majadiliano na taratibu nyingine za kidemokrasia. Nilijua kwamba kama ningeshindwa katika suala hilo, madhara yake kwa Tanzania yangekuwa makubwa sana,” anasimulia.

Hata hivyo, anasema hatukufikia hatua hiyo katika kikao hicho, kwa sababu Amour aliwashangaza kwa kuwaondolea hofu hiyo baada ya kuwaeleza kwamba, hakuwa akitafuta muhula wa tatu wa urais.

“Nafikiri Amour na wafuasi wake walitambua kwamba nilikuwa nimeazimia kutetea ukomo wa mihula miwili ya urais wa Zanzibar kwa kutumia njia zote nilizokuwa nazo Kikatiba; sidhani kama alikuwa tayari kunisukuma hadi mwisho wa uvumilivu wangu.

“Nilihisi faraja kubwa, na kila mtu alishangaa kuona kwamba, sote wawili tulitoka katika mkutano huo tukiwa na hali nzuri na moyo wa maridhiano. Ninajivunia kwamba niliweza kudumisha umoja wa nchi yangu kwa njia hiyo,” ameandika Mkapa katika kitabu chake.

Mauaji ya watu Pemba

Hayati Mkapa anaeleza katika kitabu chake kwamba mwishoni mwa Januari 2001, kulitokea janga ambalo lilimshtua na kumtikisa moyoni; polisi kuwapiga risasi na kuwaua watu 22 huko Pemba.

Wakati huo, alikuwa akihudhuria mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) huko Davos, Uswisi, hivyo Makamu wa Rais wa Tanzania wakati huo, marehemu Dk Omar Ali Juma, ndiye aliyekuwa akisimamia mambo nchini na kwa bahati pia alikuwa anatoka Pemba.

Aidha, anasema Rais mpya wa Zanzibar aliyechaguliwa wakati huo, Amani Abeid Karume naye alikuwa akihusika katika uongozi wa hali hiyo. Hata hivyo, kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anakubali kuwajibika kikamilifu kwa kilichotokea.

“Ninakiri kwamba, tukio hili daima litabaki kuwa doa jeusi katika kipindi changu cha urais, ingawa sikuwa nchini wakati janga hilo lilipotokea. Vifo hivyo vilikuwa vya kusikitisha sana.

“Hata hivyo, wakati wa taarifa zilizofuata kuhusu tukio hilo, nilihisi kwamba hakuna aliyekuwa akizingatia mazingira na shinikizo ambalo polisi walikuwa wakikabiliana nalo wakati walipoamua kutumia silaha,” anasimulia.

Hayati Mkapa anaeleza kwamba, Chama cha Wananchi (CUF) kilikuwa na ushawishi mkubwa zaidi Pemba, na wafuasi wake walikuwa wamekasirika kwa sababu hawakushinda uchaguzi, ingawa walifanya vizuri sana katika eneo hilo.

Anasema waandamanaji walidai kwamba walikuwa wakipinga tu matokeo ya uchaguzi. Hata hivyo, walimkata kichwa askari mmoja wa polisi na kisha kuelekea kituo cha polisi huku wakipiga kelele wakisema: “Tunaenda kuchukua silaha.”

“Kituo hicho cha polisi kilikuwa na ghala la silaha. Unaweza kufikiria madhara ambayo yangetokea kama waandamanaji hao waliokuwa wamekasirika wangefanikiwa kuvamia na kuchukua silaha hizo? Vurugu zilizofuata zingekuwa janga kubwa zaidi, na huenda zingesababisha vifo vingi zaidi.

“Waandamanaji hao walikabiliana na kikosi kidogo cha polisi kilichokuwa kituoni hapo, ambacho kilijibu kwa nguvu baada ya kupata msaada wa askari wengine. Tukio hilo la kutisha lilinishtua sana kwa sababu kwa kawaida watu wa maeneo ya pwani hawapendi vurugu,” anasimulia Mkapa.

Anasema hili pia halikuwa tukio lililotokea bila mazingira ya nyuma, ingawa ndilo lililokuwa baya zaidi. Kuna muhtasari wa matukio hayo uliowekwa kama kiambatisho katika hotuba aliyotoa kuhusu janga hilo.

Mambo anayojivunia

Hayati Mkapa anasema Zanzibar haikuwa na bendera yake ya Taifa tangu kuundwa kwa Muungano mwaka 1964, anafurahi kuona kwamba bendera ya Taifa ya Zanzibar ilipitishwa wakati wa uongozi wake.

Anasema suala la Zanzibar kuwa na saluti ya mizinga 21 wakati wa Maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar humweka Rais wa Zanzibar katika hadhi inayofanana na Rais wa Muungano; jambo ambalo anasema halikuwa tatizo kwa sababu mamlaka ya kila kiongozi yameainishwa wazi katika Katiba.

Anaeleza kwamba kwa vyovyote vile, mambo haya yote ni alama na taratibu ambazo wamerithi kutoka mataifa ya Magharibi.

Anahoji kwa nini Waafrika wanavipa umuhimu mkubwa kiasi hicho? Jambo la msingi ni kuwa na utawala bora na kuleta maendeleo chanya kwa wananchi.

Vilevile, Mkapa anasema alihakikisha kwamba maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanafanyika Zanzibar, jambo ambalo halikuwa limewahi kutokea kabla na lilipokewa vizuri na wananchi.

“Nilijitahidi kuhakikisha kwamba Zanzibar haisahauliki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya umma, ingawa ujenzi wa barabara kuu si suala la Muungano. Niliamua kwamba tunapaswa kutenga fedha kwa ajili ya baadhi ya miradi ya barabara Zanzibar, ili kuonyesha kwamba hali mbaya ya barabara huko Zanzibar ilikuwa pia ni jambo lililokuwa likijaliwa na Serikali ya Muungano,” anaeleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *