
Dar es Salaam. Wakati Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa akifikisha miaka sita tangu alipofariki dunia, wadau wamemwelezea kama kiongozi aliyefanya mageuzi ya kimfumo na kitaasisi huku wengine wakimtambua kama kiongozi mwaminifu na msema kweli.
Hayati Mkapa alifariki dunia Julai 24, 2020 akiwa na umri wa miaka 81 na mwili wake ulizikwa Julai 29, 2020, kijijini kwao Lupaso mkoani Mtwara.
Leo, Julai 24, 2024, imetimia miaka sita tangu kiongozi huyo alipofariki dunia huku akiacha urithi wa nchi inayoendelea kustawi kupitia misingi iliyojengwa wakati wa utawala wake, ambao ulikuwa kipindi muhimu cha mageuzi ya kiuchumi.
Mkapa katika kipindi chake cha uongozi (1995–2005), alitekeleza mageuzi makubwa ya kiuchumi yaliyolenga kujenga uchumi wa soko huria, kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuvutia uwekezaji.
Moja ya hatua muhimu ilikuwa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya Sheria Na. 11 ya mwaka 1995, ambayo ilianza kazi rasmi Julai 1, 1996.
Katika kipindi hicho, Serikali pia ilifanikiwa kushusha mfumuko wa bei kutoka asilimia 27 mwaka 1995 hadi chini ya asilimia tano mwaka 2002 kupitia sera za usimamizi wa fedha na matumizi ya mfumo wa bajeti ya fedha taslimu.
Mbali na hilo, Serikali iliongeza akiba ya fedha za kigeni kutoka kiwango kilichotosheleza matumizi ya mwezi mmoja mwaka 1995 hadi kufikia miezi 5.3 mwaka 2005, hatua iliyochangia kuimarisha uthabiti wa uchumi wa taifa na kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi.
Pia, Serikali iliimarisha mazingira ya uwekezaji kupitia Tanzania Investment Centre (TIC), kilichoanzishwa kurahisisha na kuvutia uwekezaji wa ndani na wa nje.
Wanasiasa wastaafu waliowahi kufanya naye kazi, wachumi na wachambuzi wamemwelezea Mkapa kama kiongozi aliyefanya mabadiliko wakati wa utawala wake, huku wakipendekeza viongozi wa sasa kuiga mfano wake.
Alikuwa kiongozi mkweli
Akimzungumzia hayati Mkapa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amemwelezea Mkapa akisema alikuwa kiongozi imara na shupavu, alikimwita kama “no nonsense president” (Rais asiyetaka upuuzi) na alikuwa mkweli.
Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu katika miaka 10 ya utawala wa Mkapa, amesema Mkapa alisimamia maendeleo ya nchi kwa nguvu zake zote na kwa uaminifu wote. Amesema alikuwa mtu mchapakazi kweli.
“Tunajua katika kipindi chake nchi ilivyonyenyuka kiuchumi na ilivyoheshimika katika ulimwengu wote kisiasa, kidiplomasia…kwa kweli kifo chake nchi ilipoteza kiongozi ambaye tungekuwa tunamtegemea kwa mambo mengi na watu wengi wangeiga mambo mema kutoka kwake,” amesema.
Amesema viongozi wa sasa wana mengi ya kujifunza kutoka kwake ikiwamo uaminifu, kupambana na rushwa, kuwa wakweli na kuchapa kazi kwa bidi na kusimamia maendeleo ya nchi na kila jambo jema katika nchi.
“Alihakikisha anapiga vita udhalimu wote, mambo ya rushwa na ufisadi alipambana nayo sana, alikuwa ni mtu msema kweli, kile anachosema ndicho anachotenda,” amesema Sumaye.
Alifanya mageuzi ya kimfumo
Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umasikini (Repoa), Dk Donald Mmari amesema Mkapa alifanya mageuzi ya kimfumo na kitaasisi na kuimarisha utawala wa sheria, mifumo ya uwazi ya kiserikali na kuisimamia ili kuhakikisha kwamba uongozi unajengwa na watu wenye sifa stahiki.
Amesema kwenye utumishi wa umma, ajira zilianza kutolewa kwa kuzingatia weledi ili kuchochea ufanisi serikalini, jambo ambalo halikuzingatiwa miaka ya nyuma.
Dk Mmari amesema Mkapa aliunda taasisi huru mbalimbali kama vile TRA ambayo ilikuwa ni hatua kubwa.
“Mageuzi mengi aliyafanya katika kipindi chake ya kuweka nidhamu kwenye Serikali yake. Alipenda sana kutumia ushahidi, alipenda kusoma tafiti katika kutengeneza fedha za Serikali,” amesema Dk Mmari.
Ameongeza kuwa wakati wa utawala wake, alianzisha sera ya kupambana na umasikini kwa kuanzisha Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta) ili kuwainua wananchi wa hali ya chini.
“Kweli, alijielekeza sana kwenye maeneo yale ambayo tulikuwa tunahitaji majibu, lakini pia kutumia utafiti,” amesema Dk Mmari wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu anavyomkumbuka Mkapa.
Alipambana na rushwa
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), George Kahangwa amesema utawala wa hayati Mkapa ulikuwa na mambo mengi ikiwamo kuanzishwa kwa taasisi nyingi kwa lengo la kutengeneza mfumo.
Amezitaja baadhi ya taasisi na mikakati hiyo kuwa ni Mamlaka ya Mapato (TRA), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta), Mkakati wa Kurasimisha Biashara (Mkurabita).
“Hivi leo tunapokumbuka maisha yake, moja ya vitu vya kuangalia ni pamoja na hizo taasisi, je, zinaishi ndoto yake? Zinafanya kile kilichokusudiwa kwa ufanisi na tija? Miongoni mwa vitu vinavyoangaliwa katika kumuenzi ni pamoja na hizo taasisi,” amesema.
Profesa Kahangwa amesema katika kitabu chake “My Life, My Purpose”, Mkapa anataja mauaji ya kule Zanzibar ya mwaka 2001 kama moja ya mambo hakuweza kuyasahau kwani liliitia doa Taifa.
Amesema hayati Mkapa na viongozi wa wakati ule walivuka huo wakati, kwa hiyo amesema viongozi wanaweza kujifunza kwake kwa namna alivyoweza kulivuka jambo lile na kuboresha zaidi.
Mwanazuoni huyo ambaye amewahi kugombea urais kupitia chama cha NCCR Mageuzi, amesema Mkapa hakuwa na uvumilivu katika suala la rushwa, hivyo amewataka Watanzania kujitathmini katika eneo ilo wakati wakimkumbuka Mkapa.
“Zipo nchi duniani ambazo tunaweza tukasema hazina rushwa kwa maana ya ubadhirifu wa mali za umma, lakini nchi yetu bado, taarifa za CAG zinaonyesha tuna tatizo kubwa sana kwa upande huo. Kwa hiyo kumuenzi Mkapa ni pamoja na kujitahidi katika njia ya kulipeleka taifa katika zero corruption (bila rushwa),” amesema.
Diplomasia na maendeleo
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo amesema hayati Mkapa aliingia madarakani wakati Tanzania ikikabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Amesema uchumi ulikuwa dhaifu, mzigo wa madeni ulikuwa mkubwa, na taifa lilihitaji kurejesha imani ya wawekezaji pamoja na washirika wa maendeleo.
Amesema alielewa kuwa mafanikio ya sera za ndani yangehitaji kuungwa mkono na sera madhubuti za nje. Hivyo, aliiweka diplomasia katika nafasi ya kuwa nyenzo ya maendeleo badala ya kuwa chombo cha uhusiano wa kisiasa pekee.
Katika kipindi chake, Tanzania iliendelea kujijengea heshima kama nchi yenye sera za nje zinazozingatia amani, ushirikiano na mazungumzo.
“Mkapa alikuwa kiongozi aliyependelea hoja kuliko mihemko na mazungumzo kuliko mivutano. Mtindo huo ulimwezesha kujenga uhusiano mzuri na viongozi wa Afrika na jumuiya ya kimataifa huku akiendelea kutetea maslahi ya taifa bila kuathiri misingi ya sera ya nje ya Tanzania,” amesema.
Kwa upande wa uchumi, amesema hayati Mkapa aliongoza katika kipindi ambacho mageuzi yasingeweza kuepukika.
Serikali yake ilisimamia mabadiliko yaliyolenga kuleta uthabiti wa uchumi, kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kudhibiti mfumuko wa bei, kuboresha usimamizi wa fedha za umma na kuvutia uwekezaji.
“Baadhi ya hatua zake, ikiwemo ubinafsishaji wa mashirika ya umma, zilizua mijadala na zinaendelea kutathminiwa hadi leo. Hata hivyo, hakuna shaka kwamba mageuzi hayo yalibadilisha mwelekeo wa uchumi wa Tanzania na kuweka msingi wa ukuaji katika miaka iliyofuata,” amesema mwanazuoni huyo.
Ameongeza kuwa moja ya sifa za Mkapa ilikuwa msisitizo wake juu ya nidhamu katika utumishi wa umma. Aliamini kuwa sera nzuri haziwezi kuleta matokeo bila taasisi imara, uwajibikaji na matumizi yenye tija ya rasilimali za umma.
“Falsafa hiyo bado ina umuhimu mkubwa katika mazingira ya sasa ambapo mataifa yanashindana kuvutia uwekezaji, teknolojia na mitaji ya maendeleo,” amesema Shoo.
Kuhusu mambo ambayo viongozi wanaweza kujifunza, amesema uongozi unahitaji uwezo wa kufanya uamuzi mgumu kwa maslahi ya muda mrefu ya taifa kwani historia inaonyesha kuwa baadhi ya sera zinazopingwa wakati zinapotekelezwa huweza kuonekana kuwa na manufaa makubwa miaka kadhaa baadaye.
Pia, amesema heshima ya taifa hujengwa kupitia uthabiti wa sera, uadilifu wa viongozi na uwezo wa kutekeleza ahadi. Katika dunia yenye ushindani mkubwa wa kisiasa na kiuchumi, sifa ya nchi ni mtaji muhimu unaohitaji kulindwa.