AFRIKA imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu za kiuchumi miongoni mwa nchi zake ili kuchochea maendeleo ya viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kujenga ushindani wa pamoja katika soko la dunia.
Kauli hiyo imeibuliwa katika Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayoshughulikia Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano, pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati ya Mawaziri wa Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, uliofanyika jijini Abidjan, Côte d’Ivoire.
Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, aliongoza ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika majadiliano hayo yenye lengo la kuweka misingi imara ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo endelevu barani Afrika.

Mkutano huo ulioanza rasmi Julai 24, 2026, umejikita katika kutafuta mikakati ya pamoja itakayosaidia nchi za Afrika kutumia ipasavyo fursa zilizopo, hususan katika sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji.SOMA: Waziri Mkuu: Mabadiliko ya dunia ni fursa kwa Afrika
Wajumbe wa mkutano huo walisisitiza umuhimu wa Afrika kubadilisha mfumo wa kusafirisha malighafi nje ya bara hilo na badala yake kuwekeza katika kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Hatua hiyo imeelezwa kuwa itasaidia kuongeza mapato, kuunda ajira kwa wananchi na kuongeza mchango wa Afrika katika uchumi wa dunia.
Aidha, mkutano huo umejadili umuhimu wa kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda, ambapo nchi za Afrika zinaweza kushirikiana katika uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa bidhaa ili kuongeza ushindani wa soko la ndani na la kimataifa.
Wajumbe walieleza kuwa Afrika ina uwezo mkubwa wa kuwa kitovu cha uzalishaji duniani kutokana na kuwa na rasilimali nyingi za asili, ardhi kubwa yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, madini muhimu ya kimkakati pamoja na idadi kubwa ya vijana ambao ni nguvu kazi muhimu katika maendeleo ya kiuchumi.