
Dar es Salaam. Wakati Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa akifikisha miaka sita tangu alipofariki dunia, mwanadiplomasia mkongwe, Balozi Ami Mpungwe amemwelezea kama kiongozi aliyeitoa Tanzania katika uchumi wa kizamani na kujenga uchumi wa kisasa na imara.
Mkapa alifariki dunia Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 81 na mwili wake ulizikwa Julai 29, 2020, kijijini kwake Lupaso, Masasi mkoani Mtwara.
Enzi za uhai wake, hayati Mkapa aliiongoza Tanzania kwa miaka 10 kuanzia 1995 hadi 2005 na anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika ujenzi wa uchumi, miundombinu, taasisi za udhibiti na mifumo ya kisasa ambayo manufaa yake yanaonekana hadi leo.
Leo, Julai 24, 2026, imetimia miaka sita tangu kiongozi huyo alipofariki dunia huku akiacha urithi wa nchi inayoendelea kustawi kupitia misingi iliyojengwa wakati wa utawala wake, uliokuwa katika kipindi muhimu cha mageuzi ya kiuchumi.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Balozi Mpungwe amesimulia namna alivyomfahamu hayati Mkapa na kazi aliyoifanya katika kuujenga uchumi imara na kuitoa Tanzania katika zama za ujamaa ambazo zilikuwa zimeshindwa.
Mpungwe ambaye alikuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Afrika Kusini kati ya mwaka 1994 – 1999, amesema Mkapa amewahi kufanya kazi kama Waziri wa Mambo ya Nje mara mbili, kwa hiyo anamfahamu kama mwanadiplomasia mahiri.
Amesema kazi yake ya kwanza baada ya kuhitimu masomo yake ya chuo kikuu, alikuwa mtumishi katika Wizara ya Mambo ya Nje kabla hajaingia kwenye tasnia ya habari na baadaye kuingia kwenye siasa.
Amesema yeye binafsi alikuwa karibu na Mkapa na ndiye kiongozi aliyeweza kumtambua tangu akiwa ofisa mdogo ili amsaidie majukumu katika tasnia ya diplomasia, kazi ambayo aliifanya kabla ya kuingia katika sekta binafsi.
Anamkumbuka Mkapa kama Rais wa Tanzania, ambaye amefanya mabadiliko makubwa na kuitoa Tanzania katika maisha ya kijamaa na kuingia kwenye soko huria, ili kuendana na kasi ya mabadiliko yaliyotokea duniani.
“Kwa muda mrefu nchi yetu ilikuwa inafuata mfumo wa kijamaa, mfumo wa chama kimoja, alipoingia Rais Ali Hassan Mwinyi alianza kulegeza ukiritimba wa uchumi kupitia sera yake ya “Ruksa” na pia alianzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa,” amesema.
Balozi Mpungwe amesema Mkapa ndiye Rais wa kwanza kuchaguliwa katika mfumo wa vyama vingi katika mihula yake yote miwili na yote alifanikiwa vizuri.
Amesema mzee Mwinyi alilegeza ile mibano, lakini Mkapa ndiye aliyeufanya uchumi kuwa wa kisasa kwa sababu wakati ule uchumi wa Tanzania uliathirika na sera za kijamaa, zilizokuwa za kizamani na zilizokuwa zimepitwa na wakati.
“Ilikuwa huwezi kupata bidhaa hadi upange foleni, upate vibali, lakini Rais Mkapa alipoingia madarakani, kwanza, aliimarisha macroeconomic fundamentals (misingi ya uchumi mkubwa). Nchi ilikuwa katika janga kubwa la madeni, akaweza kutunusuru kwenye mzigo huu kwa kupata yale makubaliano ya HIPC (nchi masikini zenye madeni makubwa).
“Alikwenda hadi kwenye sekta binafsi kupitia sera mbalimbali, sera kubwa aliyoiimarisha ilikuwa ya sekta ya madini. Pamoja na urithi mkubwa wa madini, tulikuwa si maarufu katika kuzalisha mazao ya madini,” amesema.
Balozi Mpungwe amesema Mkapa alianzisha Sera ya Madini ya Mwaka 1997, ikaja Sheria ya Madini ya Mwaka 1998, na wakati huo Tanzania ilikuwa ikisafirisha madini nje kwa kiwango cha sifuri, lakini kufikia mwaka 2001/02, Tanzania ilitoka kwenye sifuri hadi kufikia wazalishaji wa tatu wa dhahabu Afrika baada ya Afrika Kusini na Ghana.
Amesema sekta nyingine zilipata msukumo wa namna hiyo, jambo ambalo lilichochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania katika viwango vya juu.
Mbali na sekta kubwa, pia, alizingatia masuala la walalahoi kupitia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasiki Tanzania (Mkukuta) na Mpango wa Kurasimisha Biashara Tanzania (Mkurabita).
“Alikwenda katika nyanja zote, katika uchumi mkubwa na hata wafanyabiashara wadogo kupitia Mkukuta na Mkurabita,” amesema Balozi Mpungwe ambaye sasa ana umri wa miaka 75.
Mpungwe amesema Mkapa ndiye aliyeanzisha mamlaka za udhibiti tangu Tanzania imeingia kwenye mfumo wa soko huria, kwani kabla ya hapo ilikuwa ni vigumu kuingia kwenye soko hilo bila kuwa na sheria na taratibu, ndiyo maana mamlaka hizo, (Ewura, TCRA, Sumatra na nyinginezo) zikaanzishwa.
“Yote hayo yalifanyika katika dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa, kuutoa kwenye hali ya primitive (ya kizamani) na kuufanya kuwa wa kisasa,” amesema.
Somo kutoka kwa Mkapa
Balozi Mpungwe amesema viongozi wa sasa wana mengi ya kujifunza kutoka kwa Mkapa ikiwamo kufanya kazi kulingana na changamoto na fursa zilizopo kwa wakati husika, usikivu, msimamo na kutekeleza mambo aliyokubaliana na wadau.
Amesema anamfahamu mkapa kama mtu aliyekuwa na msimamo na alikuwa anasikiliza ushauri, akikubaliana na wewe, sawa, lakini wakati huohuo anakuwa na msimamo wake na huwezi kumyumbishayumbisha.
“Alikuwa ni kiongozi anayependa mijadala, kwa mfano, mimi wakati nimeingia kwenye sekta binafsi, yeye ndiye alihamasisha kuanzishwa kwa CEO-Roundtable na alikuwa anakaa na CEOs wa kampuni kubwa kutwa nzima na yeye mwenyewe anashika kalamu na karatasi, anawasikiliza, anaandika, anafuatilia,” amesema.
Amesema anakumbuka wakati anaisukuma sekta ya madini, mwaka 1998 mkoani Arusha, aliwaita viongozi wa kampuni zote za madini za Afrika na kwingineko, akakaa nao siku tatu akiwasikiliza kwa ujumla wao na mmojammoja.
“Ndiyo maana sekta ya madini ilipanda sana kutoka zero exporters of gold (wasafirishaji sifuri wa dhahabu) mwaka 1998 na kuwa nafasi ya tatu mwaka 2001 baada ya Afrika Kusini na Ghana.
“Kwa hiyo alikuwa ni mtu ambaye alikuwa wazi kwa mazungumzo, kupokea ushauri na majadiliano. Pia, ilikuwa mkiafikiana mnakuwa na uhakika kwamba yale mliyoafikiana atayatekeleza,” amesema Mpungwe.