
Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake huko Hague Uholanzi jana zilipiga kura kumfukuza kazi Mwendesha Mashtaka Karim Khan kufuatia madai yaliyoibua utata kwamba alimnyanyasa kingono mfanyakazi wake wa kike.
Khan, mwenye umri wa miaka 56, alisimamishwa kazi mwezi uliopita na chombo muhimu cha uongozi cha ICC kabla ya kura ya siri ambapo wanachama 82 kati ya 125 wa mahakama hiyo walipiga kura ya kumwondoa; hatua ambayo ilihitaji wingi kamili wa kura.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa ni nchi wanachama 13 pekee zilizopiga kura kuunga mkono Khan kusalia katika wadhifa wake wakati wa kikao cha faragha katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York. Nchi nyingine 15 hazikupiga kura, huku baadhi zikiwa hazikuhudhuria zoezi hilo la upigaji kura.
Mnamo Mei 2025, Khan alijiondoa katika majukumu yake ya kazi ili kupinga madai yaliyotolewa na mmoja wa wafanyakazi wenzake wa kike, kufuatia uchunguzi ulioanzishwa mwaka 2024.
Mwanamke anayedaiwa kuwa mwathiriwa, Wakili kutoka Malaysia aliyefanya kazi kama msaidizi wa moja kwa moja wa Karim Khan, alielezea tukio hilo katika mahojiano na CNN wiki iliyopita.
Wakili huyo aliyetaka kutambuliwa kwa jina lake la kwanza la Sarah aliambia televisheni ya CNN kwamba:” “Hakuna namna jambo lolote linaweza kuwa la ridhaa ya pande zote wakati kuna tofauti kubwa ya madaraka kama hiyo,” “Ninachofikiri watu wengi hawaelewi ni kwamba Bw. Khan hakuwa bosi wangu tu, bali alikuwa bosi wa kila mtu.”
Mwendesha Mashtaka huyo wa Mahakama ya ICC ambaye amekuwa katika wadhifa huo tangu mwaka 2021 amekanusha vikali tuhuma hizo.
Akizungumza kabla ya upigaji kura, Paivi Kaukoranta, Mkuu wa baraza linalosimamia mahakama ya ICC, ameitaja kesi hiyo kuwa “suala tata na nyeti la kinidhamu.”
Bi Kaukoranta ameongeza kuwa ananaamini kuwa anataraji kupata ushirikiano wa baraza linalosimamia mahakama ya ICC ili kuhakikisha kuwa wanashughuliki suala hilo kwa namna inayoheshimu kikamilifu faragha na haki za watu wanaohusika, pamoja na mahakama yenyewe kama taasisi.