Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) umepiga kura ya kumwondoa Mwendesha Mashtaka Karim Khan kufuatia madai ya utovu wa nidhamu wa kingono; timu yake ya wanasheria imethibitisha hayo, huku ikidokeza kuwa hatua hiyo ilikuwa ya “kisiasa”.

Kura hiyo ya Ijumaa imefanyika wakati ambapo ICC inakabiliwa na upinzani mkali kutoka Marekani na Israel, kufuatia hatua ya Khan kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi, Yoav Gallant, mwaka wa 2024.

Tayab Ali, Mkuu wa jopo la wanasheria wa Khan, alibainisha kuwa jopo la kimahakama lilifikia natija kwa “kwa kauli moja” kwamba matokeo ya uchunguzi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Usimamizi wa Ndani “hayakuonyesha kuwepo kwa utovu wa nidhamu au ukiukaji wa wajibu kwa upande wa Bw. Khan kwa mujibu wa mfumo husika wa kisheria”.

Mnamo Mei 2025, Khan alijiondoa katika majukumu yake ya kazi ili kupinga madai yaliyotolewa na mmoja wa wafanyakazi wenzake wa kike, kufuatia uchunguzi ulioanzishwa mwaka 2024.

Mwanamke anayedaiwa kuwa mwathiriwa, Wakili kutoka Malaysia aliyefanya kazi kama msaidizi wa moja kwa moja wa Karim Khan, alielezea tukio hilo katika mahojiano na CNN wiki iliyopita.

Wakili huyo aliyetaka kutambuliwa kwa jina lake la kwanza la Sarah aliambia televisheni ya CNN kwamba:” “Hakuna namna jambo lolote linaweza kuwa la ridhaa ya pande zote wakati kuna tofauti kubwa ya madaraka kama hiyo,” “Ninachofikiri watu wengi hawaelewi ni kwamba Bw. Khan hakuwa bosi wangu tu, bali alikuwa bosi wa kila mtu.”

Nchi wanachama ziliidhinisha kuondolewa kwa Khan takriban miaka miwili baada ya madai hayo kujitokeza kwa mara ya kwanza. Wakili huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 56 alikuwa tayari amejiondoa mwezi Juni baada ya jopo la usimamizi kuhitimisha kuwa alikuwa amefanya “utovu mkubwa wa nidhamu”.

Mwendesha Mashtaka huyo wa Mahakama ya ICC ambaye amekuwa katika wadhifa huo tangu mwaka 2021 amekanusha vikali tuhuma hizo. Akizungumza kabla ya upigaji kura, Paivi Kaukoranta, Mkuu wa baraza linalosimamia mahakama ya ICC, ameitaja kesi hiyo kuwa “suala tata na nyeti la kinidhamu.”

ICC ilisema siku ya Ijumaa kuwa ofisi ya Khan sasa itaongozwa na manaibu waendesha mashtaka Nazhat Shameen Khan na Mame Mandiaye Niang.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *