Baadhi ya wafugaji wa samaki katika Kata ya Seleli, Wilaya ya Kaliua, wameomba Serikali kuwachimbia mabwawa mapya au kuwawezesha mikopo ya kupanua mabwawa waliyonayo kutokana na msongamano wa samaki unaohatarisha uzalishaji wao.
Wakizungumza katika mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, wakiongozwa na John Masanja, wafugaji hao wamesema baadhi yao wanafuga zaidi ya samaki 1,000 ndani ya bwawa dogo, hali inayosababisha samaki kubanana, kukosa hewa ya kutosha na kuhatarisha uhai wao.
Wamesema iwapo watapatiwa mabwawa makubwa au mikopo ya kuyapanua, wataongeza uzalishaji, kupata samaki wakubwa zaidi na kuongeza kipato chao. Kwa sasa samaki mmoja huuzwa kati ya Shilingi 5,000 hadi 7,000 kulingana na ukubwa wake.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ulyankulu, Japhael Lufungija, amewapongeza wafugaji hao kwa juhudi zao na kuahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanapata mabwawa au mikopo ya kuwawezesha kupanua shughuli zao.
Amesema ufugaji wa samaki ni biashara yenye tija, ambapo mfugaji anaweza kuingiza hadi Shilingi milioni moja kwa mwaka na hivyo kuwa na sifa za kukopesheka.
Hali ya mabwawa kuwa madogo imeendelea kuwa changamoto kwa wafugaji wengi, huku mahitaji ya samaki yakiongezeka sokoni.
Uwezeshaji wa mabwawa na mikopo unatajwa kuwa njia muhimu ya kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa wananchi wa Ulyankulu.
(Feed generated with FetchRSS)