
Katika mkutano huo uliofanyika jana Jumamosi tarehe 25 Julai, Katibu Mkuu Guterres amekaribish maendeleo yaliyofikiwa katika mchakato wa mpito wa kisiasa nchini Syria na kusisitiza “umuhimu wa kuendeleza kasi hiyo kupitia ushirikishwaji wa makundi yote ya jamii.”
Guterres amesema “ushiriki jumuishi ni muhimu ili kujenga Syria yenye amani, utulivu na ustawi kwa manufaa ya wananchi wote wa Syria.”
Katibu Mkuu na Rais Al-Sharaa pia wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Syria ili kusaidia mchakato wa mpito wa kisiasa, pamoja na juhudi za kuokoa uchumi na kujenga upya nchi baada ya miaka ya mgogoro.
Aidha, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza tena dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kuheshimu na kuunga mkono mamlaka kamili ya Syria, uhuru wake, umoja wa taifa na mipaka yake inayotambuliwa kimataifa.
Pia ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu ukiukwaji unaofanywa na Israel wa Makubaliano ya Kutenganisha Vikosi ya mwaka 1974, akisisitiza umuhimu wa kulinda utulivu wa eneo la Mashariki ya Kati.
Katibu Mkuu alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa mshirika wa karibu wa wananchi wa Syria na mamlaka za nchi hiyo katika kipindi hiki muhimu cha mpito kuelekea amani na maendeleo endelevu.