
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limezionya Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu kuisaidia na kushirikiana na Marekani katika vita vyake vya jinai na uchokozi dhidi ya Iran.
Msemaji wa IRGC, Brigedia Jenerali Hossein Mohebi ametoa onyo hili leo Jumapili siku mbili baada ya Marekani kuonekana kusitisha mashambulizi yake ya anga ya mauaji dhidi ya watu wa Iran baada ya karibu wiki mbili za mashambulizi ya mabomu yaliyochochea majibu makali ya Iran.
Brigedia Jenerali Hossein Mohebi ameeleza kuwa Israel inataka kuifanya Marekani iendelee kuwepo katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa kumshawishi Rais Donald Trump na kutoa taarifa za upotoshaji, ikitumia nguvu ya Marekani kutimiza malengo yake yenyewe.
“Israel inajua tutakachofanya iwapo itarejea vitani,” ameeleza Msemaji wa IRGC.
Ametahadharisha pia kwamba kitendo cha Uingereza cha kuendelea kuunga mkono operesheni za ndege za kivita za Marekani aina ya B-1 kinaweza kuzifanya kambi za anga za Uingereza kuwa shabaha halali.
“Hivi karibuni, ndege za kivita za Marekani aina ya B-1 zilifanya operesheni kutoka katika vituo vya jeshi la anga vya Uingereza. Uingereza ikiendelea kushirikiana na Marekani tutavihesbu vituo hivyo kama shabaha zetu halali”, ameeleza Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC).
Kwa siku kumi na tatu mfululizo jeshi la Marekani limefanya mashambulizi mtawalia ya anga dhidi ya Iran na kutenda jinai za kivita kwa kushambulia maeneo ya raia na kuua shahidi watu 55.
Iran imejibu jinai za Marekani ambapo vikosi vyake vya ulinzi vimefanya mashambulizi makali ya kulipiza kisasi kwa kushambulia vutuo na kambi muhimu ya kimkakati ya Marekani kote Asia Magharibi.