
KLABU ya Simba, imetangaza kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuvunja mkataba wa kiungo mshambuliaji, Mohammed Bajaber raia wa Kenya.
Bajaber alijiunga na Simba dirisha kubwa la usajili msimu uliopita 2025-2026 akitokea Kenya Police, lakini majeraha ya mara kwa mara yalimfanya kukosa sehemu kubwa ya kuitumikia timu hiyo.
Taarifa ya klabu ya Simba imebainisha kwamba: “Kiungo mshambuliaji Mohamed Bajaber hatakuwa sehemu ya kikosi chetu kuelekea msimu mpya baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuvunja mkataba.
“Uongozi wa klabu unamtakia kheri na baraka katika maisha yake mapya ya soka nje ya Simba.”
Wakati huo huo, Simba imethibitisha kumtoa kwa mkopo wa mwaka mmoja, kiungo mshambuliaji, Saleh Karabaka kwenda Pamba Jiji.
Msimu uliopita 2025-2026, Karabaka aliitumikia JKT Tanzania kwa mkopo huku akionyesha kiwango kizuri katika kufunga akimaliza na mabao manane ya Ligi Kuu ya NBC, nyuma ya kinara wa kikosi hicho, Paul Peter aliyefunga tisa.
Kiungo huyo aliyetua Simba Januari 2024 akitokea JKU ya Zanzibar, amekuwa akitolewa kwa mkopo mara kwa mara ili apate muda mwingi wa kucheza.
Kabla ya msimu wa 2025-2026 kucheza JKT Tanzania, alikuwa Namungo aliyoitumikia kwa mkopo.