
Kocha wa timu ya soka ya Manchester City ya Uingereza kwa mara nyingine amelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya Gaza na kutoa wito jamii ya kimataifa kuwaunga mkono wananchi wa Ukanda huo ili kumaliza vita na mauaji.
Pep Guardiola amesema, “Tunashuhudia mauaji ya halaiki huko Gaza, ambapo maelfu ya watoto wamepoteza maisha na idadi hiyo huenda ikaongezeka.”Ukanda wa Gaza umeharibiwa na watu wengi wanaishi bila makazi, chakula, maji ya kunywa na dawa, aliongeza kocha huyo mahiri wa Man City raia wa Uhispania. Guardiola amebainisha kuwa, “Mashirika ya kiraia yanaweza kuwaokoa watu wa Gaza kwa kushinikiza serikali kuchukua hatua za haraka.
Hii si mara ya kwanza kwa kocha huyo wa timu ya soka ya Manchester City kuwaunga mkono watu wa Palestina; hapo awali alizungumza kuhusu haja ya kutetea haki na haki za binadamu duniani kote katika sherehe ya digrii ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha Manchester mwezi Juni.
Kocha wa timu ya soka ya Manchester City amewahi kukosoa vikali ukimya wa walimwengu kuhusiana na jinai za utawala wa kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kusema: “Ubinadamu umetoweka.” Mwezi Juni mwaka huu wakati akipokea digrii ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha Manchester, kutokana na mchango wake mkubwa ndani na nje ya uwanja kwa jiji hilo. Pep Guardiola alielezea kwa uchungu hali ya mateso ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, na kusema kuwa, ni jambo linalomuumiza sana kila anapofikiria yanayoendelea katika eneo hilo.