China imetangaza kuwa, kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ndio chanzo cha mgogoro unaoshuhudiwa hivi sasa kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Guo Jiakun amesema, hatua ya upande mmoja iliyochukuliwa na Washington ya kujitoa katika Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA) ndio chanzo hasa cha mgogoro wa sasa, na akaeleza bayana kwamba, ung’ang’anizi wa baadhi ya nchi wa “kurejeshwa vikwazo” si hatua inayojenga na inarejesha nyuma kwa nguvu kubwa mchakato wa kisiasa na wa kidiplomasia wa kutatua suala hilo.

Akizungumza siku ya Jumanne iliyopita katika mkutano wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China na wanahabari, Jiakun alisema, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilishindwa kuidhinisha rasimu ya azimio lililowasilishwa na nchi hiyo ikishirikiana na Russia la kurefusha muda wa azimio nambari 2231, na akafafanua kwa kusema: “madhumuni ya kuwasilisha rasimu ile ya pamoja yalikuwa ni kutoa muda na fursa zaidi kwa mazungumzo ya kidiplomasia kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran na kuandaa mazingira mazuri ya kufikia suluhisho kamili la kisiasa”.

Guo Jiakun

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameeleza kuwa, ung’ang’anizi wa baadhi ya nchi wa “kurejesha vikwazo” si hatua inayojenga na imerejesha nyuma kwa nguvu kubwa mchakato wa kisiasa na kidiplomasia wa kutatua suala hilo na akabainisha kwamba, Beijing inaamini kuwa utatuzi wa amani wa kadhia ya nyuklia ya Tehran unawezekana kwa njia za kisiasa tu na kidiplomasia na haikubaliani na utoaji vitisho vya namna yoyote ile kwa utumiaji nguvu au uwekaji vikwazo.

Afisa huyo wa China amesisitiza pia kuwa, Beijing ingali imefungamana na msimamo wake wa wazi  kabisa usioelemea upande wowote, na itatoa mchango wa kujenga katika kuleta suluhisho ambalo litaondoa wasiwasi wa kisheria zilionao pande zote.

Kwa ujumla, China kama ilivyo Iran inaamini kwamba, hatua ya Marekani ya kujitoa katika mapatano ya JCPOA ndio chanzo cha mgogoro wa sasa wa kadhia ya nyuklia ya Iran, na hasa kwa kuzingatia kuwa, hatua hiyo imeparaganya mlingano wa kidiplomasia na kurejesha nyuma mchakato wa utatuzi wa kisiasa wa kadhia hiyo.

Sababu za China kuchukua msimamo kuhusiana na matokeo mabaya na hasi ya kujiondoa Marekani katika JCPOA zinaweza kufupishwa kama ifuatavyo:

Kwanza ni kuvurugwa makubaliano yaliyohusisha pande kadhaa: China inaamini kwamba JCPOA ni matokeo ya mazungumzo ya muda mrefu na makubaliano ya pande kadhaa, ambapo kujitoa kwa Marekani kuliyadhoofisha na kusababisha hali ya kutoaminiana.

Pili ni kuongezeka mivutano na vikwazo: Baada ya kujiondoa Marekani, baadhi ya nchi zilijaribu kurejesha vikwazo, jambo ambalo kwa mtazamo wa China ni hatua isiyojenga na ni ya kuchochea mivutano.

Tatu ni kuidhoofisha diplomasia: China inasisitiza kuwa suluhisho pekee la kutatua kwa amani kadhia ya nyuklia ya Iran ni kutumia njia za kisiasa na kidiplomasia; na haikubaliani na utumiaji vitisho au mashinikizo. Kwa sababu hiyo, serikali ya China ilishapinga tokea awali na ikatangaza rasmi kwamba haikubaliani na vitisho vilivyotolewa na Troika ya Ulaya vya kuanzisha utaratibu wa “snapback” dhidi ya Iran na kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Hatua hiyo ya China ilichukuliwa ili kwenda sambamba na msimamo wa Iran na Russia. Beijing, pamoja na Tehran na Moscow, zilijaribu kuzuia kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Ushirikiano huo umeakisi aina fulani ya umoja wa kisiasa katika kukabiliana na mashinikizo ya Magharibi.

Kwa kuzingatia masuala hayo, China imejaribu kupendekeza rasimu kadhaa za maazimio katika Baraza la Usalama ili kudumisha anga ya mazungumzo na kuepusha kushadidi kwa mgogoro. Aidha, imetoa wito kwa Marekani na nchi za Ulaya wa kuzitaka zionyeshe uaminifu wa kisiasa na kufanya juhudi za kidiplomasia ili kuifungulia njia kadhia ya nyuklia la Iran irejeae kwenye mkondo sahihi na kuzuia kuongezeka zaidi mivutano.

Bila shaka, sura na hali ya uhusiano wa China na Iran, hususan baada ya kusainiwa makubaliano ya kimkakati ya miaka 25, nayo pia inaathiri misimamo inayochukuliwa na Beijing kuhusiana na Tehran. China inaiunga mkono Iran kwa sababu za kimkakati, kisiasa na kiuchumi…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *