
Mahakama ya kijeshi ya Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC, siku ya Jumatatu, Oktoba 6, 2025, imewahukumu watu ishirini na watatu vifungo virefu vya kuanzia miaka mitano hadi ishirini jela. Watu hao ambao walisikilizwa kwa wiki mbili, wamepatikana na hatia ya kushiriki katika harakati za uasi, njama ya uhalifu, ufadhili, na vitendo vya ugaidi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na Radio OKAPI, washtakiwa walipatikana na hatia ya kushiriki au kutoa msaada kwa mashambulizi yaliyofanywa na ADF katika maeneo ya Beni, Lubero, na Ituri.
Hukumu ndefu zaidi ilitolewa kwa Judison Kasereka Katrisa, almaarufu Kahu: miaka ishirini ya kifungo jela kwa kufadhili ugaidi na vitendo vya ugaidi. Alikamatwa mwaka wa 2018 huko Beni kwa kusimamia mtandao wa usambazaji wa ADF kati ya Butembo, Beni, na Bunia. Alihamishiwa Kinshasa, ambapo Mahakama ya Kijeshi ya Kinshasa/Gombe ilimhukumu kifungo cha miaka mitano jela mwaka wa 2021.
Kulingana na mahakama, baada ya kuachiliwa mnamo mwezi Julai 2023 baada ya kukamilika kwa kifungo chake, alirejea Bunia, ambako alisimamia mtandao mpya wa uandikishaji na usaidizi wa vifaa kwa ADF katika eneo la Tutu, takriban kilomita kumi na mbili kutoka jijini Bunia.
Akiwa anatafutwa na vyombo vya usalama, alikamatwa tena Julai 28, 2025, na kuhamishiwa Beni.
Wakati wa kukamatwa kwake, stakabadhi kadhaa zilikamatwa, ambapo baadhi zikithibitisha uhusiano wake wa hivi majuzi na ADF, pamoja na maelezo yaliyoandikwa kwa mkono yanayoelezea mapungufu ya idara za usalama wakati alipokuwa kizuizini mjini Kinshasa.