
Tukio hili limekuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) huko mjini Roma, kwa ajili ya kuinua thamani ya pamba ya Afrika na kuhimiza ushirikiano wa kitamaduni katika sekta ya mitindo.
Katika siku mbili za mwisho za mwezi Septemba mwaka huu, Alphadi pia aliendesha mafunzo kwa wanafunzi 14 wa Chuo cha Mitindo cha Roma kuhusu jinsi ya kuchanganya mitindo ya Kiafrika na ya Kiitaliano.
Alphadi, anayejulikana kama “Mchawi wa mitindo” kutokana na kazi yake ya hali ya juu ya mitindo ya kimataifa ameshirikiana na wanafunzi hao kutengeneza mavazi saba ya kipekee yaliyotengenezwa kwa kutumia pamba.
Alphadi anasema, “Kwangu mimi, hii ni njia ya kuonesha yote ambayo Afrika inaweza kufanya. Na nafikiri, hii ni njia nzuri ya kulipa heshima bara letu, na pia kuthamini kazi na kuonesha uwezo wa Afrika. Pamba ya Afrika ni bidhaa ya ubora wa hali ya juu, na inaweza kutumiwa na watu wa Sahel, pamoja na Wazungu, Wamarekani ulimwengu wote.”
Mafunzo yamekuwa mujarabu
Cecilia Marchesini, mwanafunzi wa Chuo cha Mitindo, ameeleza jinsi alivyofurahishwa na fursa hiyo ya kipekee ya kufanya kazi na Alphadi, ambaye pia ni Balozi Mwema wa Ubunifu na Uvumbuzi wa Kiafrika katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO.
Cecilia anasema, “Uzoefu huu ni wa kusisimua sana kwetu kwa sababu ni mara ya kwanza kufanya kazi moja kwa moja na utamaduni tofauti sana na wetu. Tulidhani litakuwa jambo la kufurahisha kushiriki wazo la kujipa changamoto kuchanganya tamaduni mbili tofauti ambazo mwishoni tuligundua zina mambo mengi yanayofanana.”
Mwezi Agosti 2021, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulitenga tarehe 7 Oktoba ya kila mwaka kuwa Siku ya Pamba Duniani, ili kutambua faida za kipekee za zao hilo.
Tangu wakati huo, FAO na wadau wake wameongoza juhudi za kuitangaza pamba. Mwaka huu, FAO imeshirikiana na sekta ya mitindo kuonesha safari ya pamba kutoka shambani hadi kwenye mitindo ya kisasa ikilenga kizazi kipya.
Kuhusu siu ya pama duniani
“Siku ya Pamba Duniani imeanzishwa kutokana na ombi la nchi za Afrika zinazozalisha pamba, ambazo zilipendekeza siku maalum ya kuadhimisha na kuitangaza pamba kimataifa,” amesema El Mamoun Amrouk, mchumi mwandamizi wa FAO, akiongeza kuwa “Wazo la Siku ya Pamba Duniani limetoka kwa nchi nyingi za Kiafrika zinazozalisha pamba. Walikusanyika na kuamua kwamba njia bora ya kuitangaza pamba na bidhaa yao ni kusukuma mbele Siku ya Pamba Duniani ili dunia iadhimishe pamba.”
Sekta ya pamba inawaajiri mamilioni ya watu duniani kote. Ni sekta kuu ya uchumi kwa baadhi ya nchi masikini zaidi, ikiingiza mapato kupitia mauzo ya nje.
Lengo kuu la Siku ya Pamba Duniani ni kukuza uelewa kuhusu sekta ya pamba, pamoja na kuongeza mwonekano wa mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi, biashara ya kimataifa na kupunguza umasikini, kwani pamba ni msingi wa maisha ya watu mamilioni katika zaidi ya nchi 80.