
“Katibu Mkuu Antonio Guterres amekemea vikali kukamatwa kinyume cha sheria kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, pamoja na washirika wetu, na pia wizi unaoendelea wa mali na ofisi za Umoja wa Mataifa katika maeneo yaliyoko chini ya udhibiti wa Houthi,” msemaji wake Stéphane Dujarric amesema leo akizungumza na waandishi wa habari mjini New York.
Ameongeza kuwa “Vitendo hivi vinazuia Umoja wa Mataifa kufanya kazi nchini Yemen na kutoa msaada muhimu.”
Wengi wamekamatwa
Waasi wa Houthi, wanaojulikana rasmi kama harakati ya Ansar Allah, wamekuwa wakipigana na Serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa kwa zaidi ya muongo mmoja.
Waasi hawa wanadhibiti maeneo makubwa ya nchi, ikiwemo mji mkuu Sana’a, na wamekuwa wakilenga wahudumu wa kibinadamu.
Mbali na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wanakamatwa pia wafanyakazi kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa na kitaifa NGOs, mashirika ya kiraia na balozi, wote wakiwa raia wa Yemen.
Tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza, ambavyo sasa vimeingia mwaka wa tatu, Waasi wa Houthi wamekuwa wakishambulia meli za Israeli na meli nyingine za kibiashara katika Bahari Sham, wakidai kuwa ni ishara ya mshikamano na wananchi wa Palestina.
Pia wamezindua mashambulizi ya ndege zisizo na rubani au droni na makombora dhidi ya Israel.
Wito wa kuwaachilia wafanyakazi wote waliokamatwa
Katibu Mkuu ameendelea na wito wake wa dharura kwa ajili ya kutolewa mara moja na bila masharti kwa wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa na wengine waliokamatwa, akisema lazima waheshimiwe na kulindwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Ameeleza tena kwamba wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa lazima waruhusiwe kufanya kazi bila vizuizi, na kwamba mali na ofisi za Umoja wa Mataifa zinapaswa kuwa salama na lazima zilindwe kila wakati.
“Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi bila kuchoka, na kupitia njia zote zilizopo, kuhakikisha kutolewa salama na mara moja kwa wafanyakazi wote waliokamatwa kiholela, pamoja na kurudishwa kwa ofisi za mashirika ya Umoja wa Mataifa na mali nyingine,” amesema Bwana Dujarric.
Amesema Katibu Mkuu amesisitiza kwamba “Umoja wa Mataifa anaendelea kuwa thabiti katika kujitolea kusaidia wananchi wa Yemen na matarajio yao ya amani ya haki na ya kudumu.”