
Safari yake haikuwa nyepesi. Kama wanawake wengi wanaojaribu kufaulu katika taaluma ya usafiri wa anga, Yasmin alikumbana na upinzani. Baadhi walitilia shaka uwezo wa wanawake kuendesha ndege kwa usalama.
Hata hivyo, kupitia bidii, mafunzo, na nia thabiti, aliweza kuvunja mashaka hayo yote. Chini ya uongozi na uelekezi wa mtaalamu wa usafiri wa anga, Osman Abass Amin, kupitia Maandeeq Air, Yasmin alihitimu masomo yake na kupata ujasiri wa kuwa rubani mkuu.
“Ndoto yake tangu utotoni ilikuwa kuwa rubani. Alikuwa mchapa kazi na mwenye malengo. Kama familia, tunajivunia juhudi na mapenzi yake kwa taaluma hii.
Tunamuombea kila wakati,” anasema dada yake mkubwa, Hamdi Abdi, akizungumza na TRT Afrika.
Kwa mara nyingine tena, Yasmin ametunukiwa tuzo ya Rubani Bora wa Mwaka.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Shueib Ali Warsame, alimweleza Yasmin kama “kielelezo cha ubora katika sekta ya anga ya Somalia,” na kumsifu kwa kuleta imani kwa wateja na wadau wa sekta hiyo.
“Hongera tena, Kapteni,” shirika lilitangaza kwa fahari.
Kielelezo kwa Jamii
Kwa wazazi wake, Yasmin ni baraka ya kweli.
“Yasmin amekuwa zawadi kwa familia yetu tangu alipozaliwa. Alikuwa akiongoza katika masomo shuleni na alifanya vizuri kitaaluma. Amekuwa na mchango mkubwa kwa familia na marafiki. Ni mtu wa amani, mnyenyekevu, asiyekuwa na hasira. Kama wazazi wake, tumekuwa tukimwombea yeye na familia nzima,” anasema mama yake, Habiba Bulle, akizungumza na TRT Afrika.
“Kuona akitimiza ndoto yake ya kuwa rubani ni mojawapo ya furaha yetu kuu. Alikuwa na ndoto ya kuruka angani, na ndugu zake walikuwa pamoja nasi katika kumuunga mkono. Tunaamini katika umuhimu wa kujitolea kwa ndoto za watoto wetu. Ili kufanikisha ndoto yake, tuliuza mifugo yetu na hata shamba la familia. Hilo lilikuwa bei ndogo kulinganisha na furaha ya kumuona akiruka angani,” anasema Habiba.
Sekta ya anga, ambayo hapo awali iliharibiwa na migogoro, sasa imeanza kushamiri tena.
Maboresho ya sera, teknolojia, na kurejea kwa wataalamu waliopotea vimeleta mapinduzi katika usafiri wa anga.
Ndani ya mabadiliko hayo, simulizi ya Yasmin inang’aa zaidi, si tu kwamba Somalia imejenga upya anga yake, bali pia imefungua milango kwa wanawake kuiongoza.
“Leo hii, anaendelea kuwahamasisha wadogo zake na wasichana wengine kuifuata njia yao wenyewe na kufuata ndoto zao. Tunatumai simulizi yetu itawahamasisha wazazi wote kuunga mkono ndoto za watoto wao, bila kujali gharama,” anasema mama yake.
Tuzo alizopokea; Rubani Bora wa Mwaka 2024 katika SomTex Industry Awards, na Rubani Bora wa Mwaka 2025 katika Somali Travel & Tourism Expo, ni uthibitisho kuwa mafanikio yake yanazidi kukua. Kwa wasichana wa Kisomali wanaomuona akipanda ndege, Yasmin anatoa ujumbe huu: “Kwa kila msichana wa Kisomali anayeota kuwa rubani, inawezekana.”