
Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Hamas yanafanyika katika mji wa mapumziko wa Bahari ya Shamu wa Sharm El-Sheikh, yakijikita kwenye mpango wa vipengele 20 uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump mwezi uliopita.
Rais wa Marekani Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House jana Jumanne kwamba, kuna nafasi kubwa kuwa mazungumzo hayo yanaweza kufanikisha makubaliano na akaongeza kuwa wajumbe wa Marekani pia wanashiriki katika mazungumzo hayo.
Trump ameeleza kuwa Washington itafanya “kila linalowezekana kuhakikisha kila upande unazingatia makubaliano” ikiwa Hamas na Israel hatimaye watakubaliana kusitisha mapigano.
Hamas yataka dhamana kutoka kwa Rais Trump
Mjumbe anayeongoza mazungumzo kwa upande wa Hamas, Khalil El-Hayya, amesema kundi hilo linataka “dhamana kutoka kwa Rais Trump na nchi wadhamini kwamba vita vitakwisha kabisa.”
Mazungumzo ya Misri yanajikita katika taratibu za kusitisha mapigano, kuondolewa kwa majeshi ya Israel hatua kwa hatua kutoka Gaza, na makubaliano ya kubadilishana wafungwa.
Mpango huo wa Trump umeonekana kupokelewa kwa mtazamo chanya na pande zote mbili – Israel na Hamas na umechochea kuanzishwa kwa mazungumzo yasiyo moja kwa moja yaliyoanza nchini Misri tangu siku ya Jumatatu.
Kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya nje wa Misri Badr Abdelatty, mjumbe maalum wa Trump katika eneo la Mashariki ya Kati Steve Witkoff, pia atashiriki katika mazungumzo hayo hii leo.
Aidha, mkwe wa rais Trump, Jared Kushner, aliyehudumu kama mjumbe wa Mashariki ya Kati wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, pamoja na mshauri mkuu wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Ron Dermer, pia wanatarajiwa kushiriki kwenye mazungumzo hayo.
Majed al-Ansari, ni msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar.
“Kikwazo kikubwa katika mazungumzo ya sasa ni utekelezaji wa makubaliano. Ni lazima tutafute ufumbuzi kwa njia ya vitendo ili kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa mikataba hii, kuruhusu jumuiya ya kimataifa kuingia Gaza na kuweka mifumo ya ufuatiliaji ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.”
Kwa mujibu wa chanzo cha Hamas kilicho karibu na mazungumzo hayo, utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango wa vipengele 20 wa Rais Trump bado haujakubaliwa hadi sasa.
Hamas inasisitiza kuwa, kuachiliwa kwa mateka wa Israel kunafaa kwenda sambamba na uondoaji kamili wa majeshi ya Israel.
Hata hivyo, licha ya Trump kuonyesha matumaini ya kufikiwa makubaliano, maafisa kutoka pande zote wameonyesha tahadhari kuhusu matarajio ya kufikiwa kwa makubaliano ya haraka.
Na hata iwapo makubaliano yatafikiwa, maswali yanayoibuka ni nani atakayepewa jukumu la kuisimamia Gaza na kuijenga upya, na ni nani atakayefadhili mchakato wa ujenzi mpya wa ukanda huo.
Trump na Netanyahu tayari wameondoa uwezekano wa kulikabidhi jukumu hilo kwa kundi la Hamas, jambo linaloacha pengo la kiutawala linalohitaji majibu ya haraka.