Ushindi wa Sanae Takaichi katika uchaguzi wa kiongozi wa Chama cha Liberal Democratic Party (LDP) ulipatikana baada ya kushinda duru ya pili dhidi ya Waziri wa Kilimo Shinjiro Koizumi.
Matokeo hayo ni baada ya Taro Aso mwenye umri wa miaka 85 ambaye ni mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya LDP na Waziri Mkuu wa zamani kumsaidia Takaichi katika kushawishi kura za chama.
Takaichi sasa anatarajiwa kumteua Aso, mshirika wa kisiasa wa aliyekuwa Waziri Mkuu aliyeuawa Shinzo Abe kuwa Naibu Waziri Mkuu.
Kuporomoka kwa umaarufu wa chama tawala
Wanachama wa LDP wanatumai kuwa Takaichi ataweza kuzuia kudorora kwa chama ambacho kimeitawala Japan kwa karibu kipindi chote tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Chini ya uongozi wa Shigeru Ishiba ambaye ni Waziri Mkuu wa sasa LDP ilipoteza wingi wa viti katika mabunge yote mawili kutokana na kuongezeka kwa malalamiko ya umma kuhusu kupungua kwa hali ya maisha na ongezeko la wahamiaji.
Mtangulizi wake Fumio Kishida pia kutoka LDP alijikwaa kutokana na kashfa ya michango ya fedha hali iliyozidisha mtazamo wa umma kuwa LDP haijali sana wananchi.
Baada ya ushindi wa Takaichi kiongozi mpya wa LDP aliahidi kujenga upya chama kwa kuhamasisha vizazi vyote vya Wajapan.
Mrithi wa kisiasa wa Shinzo Abe
Takaichi amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri ikiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri wa Usalama wa Kiuchumi. Akiwa na umri wa miaka 64 anajiona kama mrithi wa kisiasa wa Shinzo Abe ambaye alishinda chaguzi sita mfululizo kupitia ajenda ya kitaifa na sera za kiuchumi zinazolenga ukuaji. Anatarajiwa kuendeleza sera zake za kirafiki kwa soko na mtazamo wake wa kitamaduni kuhusu Japan.
Pia anavutiwa na Margaret Thatcher, Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Uingereza na anajiona kama “Iron Lady” wa Japan. Hata hivyo mitazamo yake mikali ya kihafidhina imekosolewa vikali na wapinzani wake huku Waziri Mkuu wa zamani Kishida akidaiwa kumwita “Taliban Takaichi.”
Ni mfuasi wa mtazamo wa kurekebisha historia ya vita na mkosoaji wa China. Hutembelea mara kwa mara hekalu la Yasukuni ambalo majirani wa Japani huliona kama ishara ya uanajeshi ingawa amekataa kusema kama ataendelea kufanya hivyo akiwa Waziri Mkuu.
Katika makala ya 2004 kwenye tovuti yake, Takaichi alitetea nafasi ya Japan katika Vita vya Pili vya Dunia akisema kuwa Tokyo ilikuwa “ikifanya vita vya kujilinda.” Alitaka kuchoma bendera ya Japan iwe kosa la jinai linalostahili kifungo.
Akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani chini ya Abe alitishia kuvipokonya vituo vya televisheni leseni zao iwapo havitaunga mkono msimamo wa serikali.
Kama Abe, anataka kuirudisha Japan kileleni kwa kukuza uchumi wake. Japan yenye watu milioni 124 kwa sasa ni taifa la nne kwa ukubwa wa uchumi duniani nyuma ya Marekani, China na Ujerumani.
Mitazamo tata
Takaichi ameshikilia mitazamo ya zamani kuhusu wanawake na usawa wa kijinsia ambayo inapendelewa na viongozi wa kiume wa chama.
Anaunga mkono urithi wa kifalme wa wanaume pekee anaona usawa wa mishahara kati ya wanaume na wanawake kama tishio kwa familia ya jadi na anaunga mkono sheria ya kiraia ya karne ya 19 kuhusu majina ya wanawake ambayo wengi huiona kama ya kizamani.
Nchini Japan wanandoa wanatakiwa kisheria kuchagua jina moja la familia na kwa kawaida mwanamke huchukua jina la mume. Takaichi alipinga mageuzi ambayo yangeruhusu wanandoa kubaki na majina yao ya awali baada ya ndoa.
Uongozi wa kivitendo au mkono wa chuma?
Hivi karibuni, ameitaka serikali kuwa na sera kali zaidi kuhusu uhamiaji, jambo ambalo limekuwa muhimu katika kampeni kutokana na kuibuka kwa chama cha Sanseito chenye msimamo mkali dhidi ya wahamiaji.
Zaidi ya hayo, Takaichi aliahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wageni na wahamiaji wanaovunja sheria kufuatia ongezeko la wageni Japan ambayo kwa kawaida ni jamii yenye mfanano mkubwa.
Kiongozi mpya anatarajiwa kugeuza mwelekeo wa kuporomoka kwa umaarufu wa LDP kwa kuwavutia wapiga kura wa vyama vya mrengo wa kulia. Takaichi pia alikubaliana na upinzani kuwa ataondoa kodi ya petroli ya miaka 50 kipaumbele katika kukabiliana na mfumuko wa bei.
Alisisitiza pia haja ya kuwa na jeshi imara, akieleza umuhimu wa ushirikiano wa pande tatu kati ya Japan, Marekani na Korea Kusini na hivyo kupunguza hofu kuwa mahusiano yaliyorekebishwa na Seoul yanaweza kuharibika tena kutokana na msimamo wake wa kitaifa.