Maonesho yako kwenye uwanda wa wageni nje ya jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani yakiwa ni picha zilizopigwa na wanawake kutoka Haiti, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) Sudan, Lebanon, Palestina, Kosovo, Msumbiji na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
Wanawake wanasaidia kuonesha taswira tofauti ya DRC
Kutoka DRC ni Do Nsoseme Dora ambaye anasema kile ambacho kimemsukuma kuwa mpiga picha za wanawake wanaofanya harakati za kuleta amani ni kwamba “tunapoangalia katika historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na miaka ya vita na mapigano ya kijamii, mara nyingi tunasahau simulizi za wanawake ambao husababisha watu kwenda kwenye meza kwa ajili ya kusaka amani.”
Anasema wanawake wanasaidia kuonesha taswira tofauti ya DRC na kuleta simulizi ambazo mara nyingi huwa zinasahaulika.
Picha aliyopiga ni ya Nelly Mbangu, mwanasheria na wakili kutoka jimbo la Kivu Kaskazini huko mashariki mwa DRC.
Bi. Mbangu anasema “licha ya kukumbwa na vitisho na kufurushwa huku na kule anafanya kampeni kutetea haki za wanawake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na watoto na wanawapatia msaada wa sheria.”
“Iwapo utaelewa na kuamini katika nguvu na uwezo wako katu hutopoteza. Baada ya ghasia kuna maisha na hivyo basi kama kuna maisha kuna matumaini,” ndio kauli ya Bi. Mbangu kupitia picha aliyopigwa na Dora.
Wapiga picha wanawake waonesha harakati amani za wanawake mashinani.
Ulemavu wa viungo si kikwazo
Dora amepiga pia picha ya Melanie Kabamba. Huyu ni mwandishi wa habari na ni mwanamke mwenye ulemavu wa viungo ambaye pia ni mtetezi wa haki za wanawake wenye ulemavu nchini DRC.
Bi. Kabamba ni Rais wa Kituo cha Wanajamii na watu wanaoishi na Ulemavu na yeye anatetea ushiriki wa watu wenye ulemavu katika siasa na harakati za kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali.
Katika bango lenye picha yake, nukuu ambayo imewekwa katika picha yake Bi Kabamba ni kwamba, “mimi ni mwanamke ninaishi na ulemavu. Ninajivunia kwa sababu ulemavu si viungo bali ni wa kifikra. Na kama fikra zako zimemakinika na unajitambua mwenyewe kama ni mtu ambaye unaishi kama watu wengine.”
Fanyia kazi kinachokuchukiza ili kuepusha wengine
Bango lingine lina picha zilizopigwa na Alice Ambrucer kutoka Msumbiji. Alice ni Afisa mradi na pia mpiga picha wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women nchini Msumbiji.
Kwa mujibu wa Alice, “zingatia kile ambacho kinakuchukiza wewe na vile ambavyo kinaweza leta madhara kwa watu wengine. Angalia jambo hilo nyumbani kwako katika jamii yako na dunia nzima kwa jumla na kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko.”
Alice anasema iwapo kila mtu atatekeleza wajibu wake, basi unaweza kuleta mabadiliko makubwa.
Picha aliyopiga ni ya Maria ambayo anaongoza harakati za mashinani katika jimbo la Cabo Delgado lililogubikwa na machafuko.
Lengo la harakati zake Maria ni kuepusha au kuzuia utumikishwaji wa watoto. Nukuu ya Maria kwa mujibu wa picha aliyopigwa na Alice ni “niliamua kufanyia kazi eneo hili kwa sababu niliona pengo kubwa. Kulikuwa hakuna mtu wa kuzungumza kwa niaba ya wanawake. Wakati wanawake walikuwepo katika mikutano, tulihisi kwamba walikuwa wanaogopa kuzungumza kwa hofu ya kukumbwa na visasi kutoka kwa waume zao.”