Duru mbalimbali za kieneo zimeripoti mepema leo Alkhamisi kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kufanya mashambulizi makali katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Ghaza licha ya kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita.

Shirika la Habari la Fars limeripoti kuwa; licha ya kutangazwa makubaliano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Ghaza kati ya utawala wa Kizayuni na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, lakini Israel inaendelea kufanya mashambulizi makali kwenye ukanda huo uliozingirwa kila upande. 

Mwandishi wa televisheni ya Al Jazeera ameiripoti kuwa mizinga ya jeshi la kigaidi la Israel inaendelea kushambulia maeneo mbalimbali ya Ghaza.

Hayo yamekuja huku muda mfupi tu nyuma, rais wa Marekani Donald Trump alikuwa amedai kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita Ghaza. Hata Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar na HAMAS nazo zilikuwa zimetangaza kutiwa saini makubaliano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Ghaza.

Katika taarifa yake ya mapema leo Alkhamisi, Hamas sambamba na kuthibitisha kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha vita imesema kwamba makubaliano hayo yatamaliza vita dhidi ya Ghaza, wavamizi watatimuliwa na kutakuwa pia na kubadilishana mateka.

Sehemu moja ya taarifa ya HAMAS imesema: “Tunatangaza rasmi kufikiwa makubaliano ambayo yatawezesha kumalizika uvamizi wa Ghaza na kubadilishana mateka kufuatia mazungumzo yenye uwajibikaji na mazito kati yetu na makundi ya Muqawama ya Palestina kuhusu pendekezo la Trump huko Sharm el-Sheikh la kumaliza vita vikali dhidi ya watu wa Palestina na kuondoka wavamizi katika Ukanda wa Ghaza.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *